Wednesday 26 July 2017

LOWASSA ATIKISWA NYUMBANI KWAKE


JINAMIZI la madiwani wa CHADEMA kujiuzulu katika mkoa wa Arusha, limebisha hodi nyumbani kwa mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa, ambapo diwani wa Kata ya Moita, Wilaya ya Monduli, Saimon Sapunyu, amejiuzulu wadhifa wake na kujiunga na CCM.

Akithibitisha kujiuzulu kwa Sapunyu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Steven Ulanga, alikiri kupokea barua ya diwani huyo jana.

Ulanga alisema katika barua hiyo, diwani huyo alitaja sababu kubwa ya kujiuzulu kwake kuwa ni kutokuwepo kwa demokrasia ndani ya CHADEMA na amekunwa na utendaji kazi mzuri wa Rais Dk. John Magufuli.

"Ni kweli nimepokea barua ya diwani wa kata ya Moita kujiuzulu, nitaiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya kutangaza tarehe nyingine ya uchaguzi,"alisema Ulanga.

Kwa upandewake, Sapunyu alisema ameamua kurudi CCM kutokana na CHADEMA kutokuwa na demokrasia.

Alifafanua kuwa, kumekuwa na urasimu wakati wa kuendesha vikao vya halmashauri kutoka kwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga na Mwenyekiti wake, Joseph Issack.

"Ndani ya CHADEMA nilikuwa naelewana na madiwani wenzangu, lakini nilikuwa sielewani na mwenyekiti wa halmashauri na mbunge, kutokana na urasimu ndani ya vikao na wakati mwingine kukwamisha miradi ya maendeleo kwa makusudi katika kata yangu, ukiwemo mradi mkubwa wa maji na ukarabati wa shule ya wasichana ya Kipok," alisema.

Akitolea mfano, alisema mradi mkubwa wa maji uliokuwa unatoka eneo la Magereza kwenda kwenye kata yake, umekuwa ukisuasua licha ya kutengewa fedha

Aliongeza: "Wananchi wanapata adha kubwa ya maji. Hii imekuwa
changamoto kubwa kutokana na mwenyekiti wa halmshauri na mbunge kutosimamia kikamilifu. Na baada ya kukwama, nililazimika kuomba msaada kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru na Monduli, ambao walinisaidia kwa kiasi kikubwa na sasa mradi unakwenda vizuri."

Sapunyu, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mpaka 2015, alisema sababu nyingine iliyomfanya kurudi CCM ni utendaji kazi wa Rais Dk. Magufuli, ambaye amejitoa kwa ajili ya Watanzania wanyonge.

"Nilikuwa CHADEMA, nikachukuliwa na mafuriko, nimejitambua, nimeamua kurudi CCM ili niweze kumuunga mkono Rais wangu na kuendelea kuwatumikia wananchi wa kata ya Moita, nikiwa mwananchi wa kawaida,"alisema.

Kujiuzulu kwa Sapunyu, kumefikisha idadi ya madiwani wa CHADEMA waliojiuzulu katika mkoa wa Arusha kufika tisa.

No comments:

Post a Comment