Wednesday 26 July 2017

TUMEUMIZWA UBINAFSISHAJI-JPM



RAIS Dk. John Magufuli amesema baadhi ya hatua za ubinafsishaji zilizochukuliwa na serikali miaka ya nyuma, zimewaumiza Watanzania badala ya kuwasaidia.

Kutokana na kasoro hiyo, Rais Magufuli ametaka ijengwe tabia ya kutokubali kila kinacholetwa kutoka nje.

Alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akifungua barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya, yenye urefu wa kilomita 89.3, wilayani Itigi mkoani Singida.

Rais Magufuli alisema katika ubinafsishaji, Tanzania imeumia na kwamba isingefanya hivyo, isingehangaika kujenga viwanda vipya hivi sasa.

Alisema wale waliokabidhiwa viwanda kwa ajili ya kuviendeleza, wameshindwa kufanya hivyo, matokeo yake viwanda hivyo vimegeuzwa kuwa magodauni.

"Tulikuwa na kiwanda cha matairi, lakini leo hakipo, tukawapa wawekezaji wakakiua, wakaenda kufufua nchi jirani kiwanda chao, halafu wanatuletea sisi matairi," alisema.

Alisema halipendi suala la ubinafsishaji kwa sababu kuna viwanda zaidi ya 197, vimebaki magodauni kutokana na kutelekezwa.

"Nenda Morogoro, nenda Mwanza, Urafiki tulikuwa na mashine ya kusagia mazao, tukawauzia watu, wakang'oa na kupeleka nchi jirani. Tulifikia hapo na waliotudanganya ni hao hao wazungu," alisema.

Aliongeza:"Uende hata Ujerumani, hawabinafsishi viwanda vyao, sisi walitaka hata reli tuibinafsishe wakati wao hawafanyi hivyo. Mashirika yao ni yao, umeme wao, sisi kila kitu tunabinafsisha, tunaingia ubia na matapeli.

"Wengine mtashangaa mbona huyu Rais anaongea haya, ni lazima niyatapike, vinginevyo nitapata presha. Na nikiyatapika, wale walioyafanya lazima wakumbuke kuwa kuna mtu anatapika dhambi zao."

Rais Magufuli pia, aliwataka Watanzania kuacha kupokea kila kitu wanacholetewa na wawekezaji kwa sababu siyo vyote ni vizuri.

"Siyo kila kitu tunacholetewa ni kizuri, vipo vinavyoletwa vya ajabu kwa hiyo ni lazima Watanzania tujifunze kukataa, tuvikubali vile ambavyo ni vizuri vya hovyo tuvikatae kwa nguvu zote," alisisitiza.

Alisema: "Haingii akilini tuwe na pamba yetu, tunailima, wanainunua hapa, wanaenda kutengeneza nguo, halafu wanazivaa, baadaye wanatuletea hapa eti mitumba."

Aliongeza: "Sasa lazima tubadilike, tuwe na viwanda, tulime pamba yetu, tutengeneze nguo zetu, tuvae, halafu tukizichoka tuzifunge kwenye marobota na tuwapelekee huko nao wakavae."

Vilevile, alisema anataka Tanzania iwe ya viwanda, hivyo ametoa maagizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na wajue mapema vitakuwa vya aina gani.

"Zungumzeni na wawekezaji, zungumzeni na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ili wawekezaji mbalimbali waje kuwekeza Singida," alisema.

Aliongeza: "Nilikuwa mkoa wa Pwani, uongozi wake umeweza kuwa na viwanda 371, vikubwa 81, wametumia nafasi zao."

Akizungumzia kiwanda cha Tanganyika Packers, alisema: "Haya mashamba yaliyokuwa ya Tanganyika Packers, nyinyi mnataka muyagawe, muyalime lakini ungekuwa mkoa unaojua kujipanga vizuri, hapo ndiyo wangeweka mahali pa kujenga viwanda."

Rais Magufuli alisema watakapokuwa na viwanda, vijana wote wa Singida watapata ajira na uchumi utaimarika. Pia, aliwashauri wananchi wa Singida, kulima alizeti ya kutosha ili wawekezaji wapate nguvu ya kuja kuwekeza mkoani humo.

"Kuna kiwanda kikubwa, lakini kinalalamika hakipati alizeti ya kutosha, limeni ndugu zangu," alisisitiza.

AHOJI KUHUSU BIL 104/-

Rais Magufuli alisema anafahamu kuna mradi wa barabara kutoka Mkiwa-Itigi-Makongorosi, hivyo lazima itengenezwe kwa kiwango cha lami ili kuufanya mji huo uwe wa aina yake.

"Tumetangaza tenda na tupo kwenye mchakato wa kumpata mkandarasi, lakini nataka nimueleze waziri, katibu mkuu na TANROADS, tunaanza na kilomita 57, gharama naona ni sh. bilioni 104, haiwezekani," alisema.

"Kwa maana nyingine, kilomita moja inajengwa kwa gharama kubwa zaidi ya bilioni moja, nataka TANRODS mzipitie hizo gharama upya. Wakati mnajadiliana na mkandarasi, hizo mlizozipanga akikubali, anayetaka kujenga mmuongeze eneo, siyo kilomita 57, ziendelee mbele zaidi. Akikataa punguzeni hizo fedha muwe na kiwango kinacholingana na kilomita 57. Nataka kuwe na matumizi bora ya fedha," alisema.

Pia, alisema alipokuwa waziri wa ujenzi, alimfukuza kazi Mkurugenzi Mtendaji wa TANROADS, kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha katika ujenzi wa barabara.

Kutokana na hali hiyo, alimuomba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuwa makini ili asitumiwe na TANROADS.

"Katika wizara, ambayo nataka muhakikishe kuwa sijatoka, ni wizara ya ujenzi. Nafuatilia kila kitu kwa sababu ninajua fedha ninazozitoa kwa kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Msije mkadanganyika, mkaleta masuala ya yule mkurugenzi mtendaji niliyemfukuza ndani ya siku tatu, tena ilikuwa siku ya Jumapili, siku ya Mungu," alisema.

Alisema katika mradi huo, lazima wapitie upya makubaliano na mkandarasi huyo ili barabara hiyo ijengwa kwa gharama inayotakiwa.

"Na hawa wakandarasi wajifunze. Zamani walikuwa wanaweka gharama kubwa kwa sababu hawakuwa na uhakika wa kulipwa fedha. Leo fedha ipo, hawawezi kuwa wanaweka gharama za juu.

"Barabara hii hakuna madaraja makubwa, mimi naijua, huwezi ukaweka shilingi bilioni 104 na kilomita 57, haiwezekani. Mkurugenzi Mtendaji umenielewa? Na ninalisema kwa dhati, sitasubiri kufukuza mtu mpaka afukuzwe na waziri, ninakufukuzia huko huko juu. Sasa isije ikafikia hapo, bado nawapenda TANROADS na mnafanyakazi nzuri," alisema.

AWAASA WATANZANIA

Rais Magufuli pia aliwaomba Watanzania kuilinda na kuitunza vyema amani ya nchi yao kwani palipo na amani, kuna maendeleo.

"Uchumi wa nchi yetu ni mzuri, unakuwa kwa asilimia saba, ni miongoni mwa nchi tano katika Afrika, ambazo uchumi wake unakwenda kwa juu, tukiongozwa na Ivory Coast. Tumepanga uchumi ukue kutoka asilimia saba, ifike hadi asilimia 7.1," alisema.

Kwa upande wake, Profesa Mbarawa alisema barabara hiyo ni muhimu kwa mikoa ya Singida, Tabora na Kigoma kwa sababu ni sehemu ya barabara kuu ya kutoka Tabora hadi Manyoni.

Alisema barabara hiyo, ambayo imegharimu sh. bilioni 114.692, itafungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wanaoishi katika mikoa hiyo.

No comments:

Post a Comment