Wednesday 26 July 2017

WABUNGE WALIOTIMULIWA CUF BADO HAKIJAELEWEKA



SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ameweka kiporo kutoa msimamo kuhusu kusimamishwa kwa wabunge wanane wa viti maalumu wa chama cha Civic United Front (CUF).

Hatua hiyo inafuatia kupokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Kaimu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya, kuhusu uamuzi wa baraza kuu la chama hicho kuwafukuza viongozi hao.

Barua hiyo iliwataja waliofukuzwa uanachama kuwa ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mwassa, Riziki Ngwali, Raisa Mussa, Miza Haji,  Hadija Al-Qassmy na  Halima Mohamed,

Pia, imeainisha makosa yao kuwa ni kukiuka kifungu cha 83(4) na (5) cha katiba ya chama hicho kwa kutenda makosa, ikiwemo kukihujumu katika uchaguzi wa marudio wa madiwani wa Januari 22, mwaka huu, kumkashifu na kumdhalilisha Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Lipumba, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena na wakurugenzi wa chama hicho.

Makosa mengine ni kushirikiana na CHADEMA katika kupanga operesheni waliyoiita 'ONDOA MSALITI BUGURUNI', wakiwa na lengo la kumuondoa Mwenyekiti halali wa chama hicho kinyume na taratibu za Katiba ya CUF na Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992.

Barua hiyo imeyataja makosa mengine, ambayo viongozi hao walifanya kuwa ni kuruhusu na kuipa fursa CHADEMA, kuwa msemaji wa masuala ya CUF kinyume na matakwa ya Katiba ya CUF, kulipia pango na kufungua ofisi ya CUF Magomeni bila kufuata taratibu.

Makosa mengine ni kuchangia fedha kukodisha watu kwa lengo la kuwadhuru viongozi watiifu wa chama, akiwemo Profesa Lipumba, Magdalena na mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma.

Hata hivyo, Spika amesema suala la kuwaondoa uanachama wabunge hao ni la utashi wa vyama vyenyewe na kila chama kinao utaratibu wake.

"Hivyo bado naendelea kuitafakari barua hiyo na taarifa rasmi kuhusu maamuzi ya Spika kwa wabunge waliofukuzwa, nitaitoa baadaye," ameeleza Spika Ndugai kwenye barua hiyo.

No comments:

Post a Comment