Wednesday 26 July 2017

KUKAMATA VIONGOZI WA DINI, WANASIASA SIYO KOSA-IGP


JESHI la Polisi nchini limesema, linapowakamata wanasiasa au viongozi wa dini, halifanyi hivyo kwa sababu ni viongozi wa chama fulani au dhehebu fulani, bali ni kwa sababu ya uhalifu.

Limesema kutokana na sheria za nchi, mwanasiasa ama kiongozi wa dini anapojiingiza kwenye uhalifu, huwa ni mhalifu na atashughulikiwa kama mhalifu.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Mara na Mwanza.

"Naomba Watanzania waelewe, IGP anatuma watu wake kwenda kumkatama mhalifu kwa kosa fulani, simkamati padri kwa sababu ni padri. Sitegemei padri anaweza kujiingiza kwenye uhalifu, akishajiingiza kwenye uhalifu ni mhalifu. Tunashughulika naye kama mhalifu," alisema IGP Sirro.

Aliongeza: "Sheikh naye ni hivyo hivyo, akifanya uhalifu, tunamkamata kama mhalifu, hatumkamati kama Sheikh. Tunaomba hili lieleweke."

IGP Sirro alisema pia kuwa, inapotokea mwanasiasa amekamatwa na polisi kwa kosa fulani, awe wa chama tawala au upinzani, wananchi wanapaswa kujua kuwa, amekamatwa kwa sababu ana tuhuma za uhalifu.

Alisema baada ya jeshi hilo kufanya upelelezi na kubaini kuwa, mtuhumiwa hana hatia, ataachiwa mara moja, lakini iwapo itabainika kwamba upo ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma zinazomkabili, atafikishwa mahakamani.

"Lakini kikubwa tunawaomba wananchi watusaidie kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu," alisisitiza Kamanda Sirro.

Aliongeza kuwa, wakati serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ikiwa imedhamiria kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020, ulinzi wa rais na mali zao lazima uimarishwe.

"Tunapambana kwenda kwenye uchumi wa kati na serikali imeadhimia kujenga Tanzania ya viwanda. Hatuwezi kuwa na viwanda vingi iwapo hakutakuwepo na amani nchini. Hilo litawezekana kama nchi itakuwa na amani,"alisisitiza.

Wakati huo huo, IGP Sirro, amewataka askari wa jeshi hilo kuhakikisha wanatenda haki wakati wakitekeleza majukumu yao ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu.

Aidha, IGP Sirro, ametoa wito kwa wananchi na raia wema, kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kudhibiti matishio mbalimbali ya uhalifu yanayoweza kujitokeza katika maeneo yao.

IGP Sirro, aliyasema hayo juzi, akiwa kwenye muendelezo wa ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza.

Wakati wa ziara hiyo, pia alipata nafasi ya kuzungumza na askari wa jeshi hilo, ikiwa ni pamoja na kujitambulisha kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.

No comments:

Post a Comment