Wednesday 9 September 2015

KIBAJAJI AMPA LOWASSA DOZI KUBWA

NA PETET KATULANDA, SIMIYU

MJUMBE wa Kamati ya Kampeni ya CCM taifa, Livingstone Lusinde, ameitikisa mjini Bariadi na kusema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa hawezi kuleta mabadiliko ya kweli Tanzania wakati mwenyewe ameshindwa kubadilika.

Alisema moja ya Kanuni ya Uchaguzi Mkuu si kuchagua sura ya mgombea, ni pamoja na kuchagua ilani ya chama na sera zake, ndiyo maana CCM imeleta watu safi akiwemo mgombea urais Dk. John Magufuli na kitabu (Ilani) chenye sera nzuri.
Lusinde maarufu kama ‘kibajaji’ pia ameionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa isipokemea tabia za baadhi ya wagombea wanaomba kura kanisani wakitaka upendeleo wa udini, umoja wa kitaifa utasambaratika.

Aliyasema hayo juzi wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Bariadi na vitongoji vyake wakati wa ufunguzi wa kampeni za CCM mkoani hapa uliofanyika kwenye viwanja vya CCM.

“Lowassa anasema tunataka mabadiliko wakati yeye ameshindwa kubadilika na kamwe hatoweza kubadilika na kuacha ufisadi, angekuwa anaweza kubadilika asingethibitisha ufisadi wake kwa kununua chama kizima kizima na kuwaziba mdomo kina Mbowe,” alisema na kuamsha shangwe ya umati uliofurika uwanjani hapo.

Baadaye aliuchekeza umatu huo pale alipodai kuwa: “Tunachagua wawakilishi kata, majimbo na kiongozi mkuu wa nchi, Lowassa amelifilisi taifa leo anataka kuwa Amiri Jeshi Mkuu, hilo gwaride atalikaguaje wakati hawezi hata kuwahutubia wananchi kwa dakika 20 ?, Juzi alihutubia dakika sita.”

Alifafanua kuwa, kila jambo duniani lina kanuni yake, hata nguo zina kanuni ya kuvaa, hakunammtu anayeweza kuvaa suluali kupitia mikononi hivyo hata kanuni ya Uchaguzi Mkuu ni kuchagua chama kilichopangwa vizuri, Ilani yake na mgombea safi, siyo sura ya mgombea au mahaba yake.

Alidai, UKAWA wamepachika watu, mgombea wao wa urais hana ilani ndiyo maana kila kukicha anasahau hili na kukurupuka na lile, lakini CCM imeleta mtu safi na ilani bora, Dk. Magufuli anakuja kubadili mfumo wa serikali na Chama, wazembe na mafisadi watatimuliwa.

Alilalamikia siasa za kuomba kura makanisani zitaliangamiza taifa na kuionya NEC ikemee jambo hilo haraka. “Tunataka mtu wa kwenda Ikulu kuchapa kazi siyo kuuguza, sasa ameanza kuomba kura kanisani.”

“Eti, naomba mniombee, mniombee kweli kweli nyie walutheri mna sababu ya kuomba zaidi sababu nchi hii tangu iumbwe haijapata kutoa rais Mlutheri, Mwalimu Nyerere alikuwa Mkatoliki, Mkapa Mkatoliki, Mungu atatuongoza nasi tupate nafasi hiyo…” alisema akimuigiza Lowassa na kuwavunja mbavu wananchi.

Kibajaji alihoji nani asiyejua kuwa Lowassa na Frederick Sumaye na mawaziri wakuu wengine waliotoka kanda ya kaskazini ni Walutheri, lakini wananchi hawajawahi kulalamika makanisani na misikitini.  “Kama Lowassa anasema hivyo na sisi Wagogo tukisema hii zamu yenu wasukuma, tunawaunga mkono wasilalamike.”

Awali, akimkaribisha Lusinde kuhutubia wananchi na kuzindua kampeni hizo, Mwenyekiti wa CCM mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani alisema wana CCM na wananchi wapenda maendeleo wa mkoa huo na taifa kwa ujumla wachague wagombea wa CCM ili wapate maendeleo.

“Ili CCM ishinde chagueni mafiga matatu mkianza na Dk. Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM, Simiyu ilikuwa ngome ya wapinzani maana kati ya majimbo saba, matatu tu ndo yalikuwa ya CCM sasa makundi Simiyu yamekwisha, tushikamaneni tushinde, utemi bado ni wa CCM,” alisema Dk Kamani.

No comments:

Post a Comment