Wednesday 9 September 2015

CCM YAONYA, YASEMA KULIGAWA TAIFA KWA MISINGI YA DINI HAIKUBALIKI




NA MUSSA YUSUPH
MGOMBEA urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa, ameendelea kukaliwa kooni kwa kitendo chake chenye dhamira ya kuliwaga taifa cha kuomba kura kwa misingi ya kidini akiwa kanisani.
Lowassa, Jumapili iliyopita mkoani Tabora, akiwa kwenye ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) aliwashawishi waumini wa kanisa hilo kumchagua kuwa rais kwa sababu yeye ni muumini wa dhehebu la Kilutheri.
Akiwa kwenye ibada hiyo, Lowassa ambaye ni waziri mkuu aliyejiuzulu kutokana na kukabiliwa na kashfa, alisema tangu kuumbwa kwa nchini hii, Tanzania haijawahi kuongozwa na rais wa dhehebu la Kilutheri.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kauli ya Lowassa ililenga kuligawa taifa kwa misingi ya kidini.
Alisema alichokifanya Lowassa, kinakwenda kinyume na mila na desturi za Kitanzania, sheria za uchaguzi pamoja na kanuni za maadili ya uchaguzi zilizotiwa saini na vyama vyote vya siasa.
Nape alisema maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015 yaliyotolewa kupitia  tangazo la serikali namba 294 Julai 27, mwaka huu, yanakataza viongozi wa kisiasa au wafuasi wao kufanya kampeni kwenye nyumba za ibada.
“Kifungu cha 124 (a) cha sheria ya taifa ya uchaguzi sura ya 343 kifungu 2.1 (k) kinasema, viongozi wa vyama vya siasa, wagombea au wafuasi wao wanapaswa kuhakikisha kuwa majengo wanayoyatumia kufanyia Kampeni yasiwe ya ibada” alisisitiza.
Alisema kifungu hicho pia kinawataka kutotumia viongozi wa dini kuwapigia kampeni au kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya dini, ukabili au rangi.
Nape ambaye ni mgombea ubunge kupitia CCM, jimbo la Mtama, alisema kwa sababu tabia ya kusahau inazidi kuongezeka kwa Lowassa, ni vyema akaelezwa kanuni hizo.
Pia, kauli hiyo imethibitisha kuwa CHADEMA na kundi la UKAWA, wanaendesha siasa za kibaguzi, uchochezi na waroho wa madaraka wasiojali maslahi ya nchi.
Aliongeza kuwa kauli hizo si mara ya kwanza kwa CHADEMA na Lowassa kuendesha siasa za kibaguzi ambapo awali, walitumia sera ya ukanda na sasa wanatumia dini kama njia ya mkato ya kutafuta madaraka.
Katibu huyo wa uenezi wa CCM, alisema tabia hiyo sio utamaduni wa Watanzania bali ni uroho binafsi wa madaraka wa Lowassa na CHADEMA baada ya hoja zake kukataliwa na wananchi.
Alisema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuonya kuwa wanasiasa wanaotumia dini na ukabila kama hoja ya kusaka madaraka wamefilisika kisiasa na ni watu hatari kwa mustakabali wa amani na mshikamano wa taifa.
Kauli hiyo ya Lowassa, alisema imelaaniwa na CCM na inapaswa kulaaniwa na watu wote hasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua hatua stahiki dhidi yake.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kuchukua hatua zinazostahili kuondoa mbegu ya kansa inayoletwa nchini, maneno ya Lowassa ni kansa mbaya na lazima yakemewe na kukomeshwa,” alisema.
Aliongeza kuwa tabia ya ubaguzi ndiyo iliyomfanya Lowassa kukosa nafasi ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM kwa sababu Chama Cha Mapinduzi hakiamini katika ubaguzi.
Akiwa kanisani Lowassa alisema:  “Naomba mniombee, mniombee kweli kweli. Nyie Walutheri mnasababu ya kuomba zaidi kwa sababu tangu nchi hii iumbwe, haijapata kutoa Rais Mlutheri. Mwalimu Nyerere alikuwa Mkatoliki, Rais (Benjamini) Mkapa alikuwa Mkatoliki. Sasa nadhani Mungu atatuongoza ili nasi tuweze kuipata nafasi hiyo. Kwa hiyo naomba mniombee sana.”
WASOMI WASEMA KOSA
HILO HALISAMEHEKI
Kwa  upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Benson Bana, alisema Tanzania haina dini na maendeleo yaliyofikiwa hayakuletwa na dini yoyote, hivyo hatua ya Lowassa kutangaza udini katika kuomba kura ni kosa lisilosamehewa.
Alisema waachwe Watanzania wampime kila mgombea kwa sera zake na suala la dini lisipewe nafasi kwa kuwa ni hatari.
“Ni mwendelezo wa siasa zilezile za ukanda na udini na Watanzania hawataki kusikia kauli za kuwagawa ni wazi mgombea huyo amepoteza tunu za taifa na washauri wake ndio wanaompoteza zaidi,” alisema.
Dk. Bana alisema si jambo jema kiongozi kuwagawa wananchi kwa udini na kushauri kuwa Lowassa anapaswa kuheshimu maadili.
Akizungumzia kampeni zinazoendelea alisema ni wazi vyama vya siasa vimejipanga na vinafanya kampeni zake kistaarabu,  hivyo wagombea ni vizuri kuchunga ndimi zao na kuheshimu sheria, taratibu na maadili ili kulinda amani ya taifa.
NEC YAKEMEA VIKALI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa mara nyingine imewakumbusha  wagombea na vyama vyao kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ambayo walikubali kuyafuata

“Inasikitisha kuona kiongozi au mgombea anatumia madhabahu kufanya kampeni na mbaya zaidi kuomba kura kwa misingi ya kidini.  Kitendo kilichofanywa na mgombea wa CHADEMA, Lowassa kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri kumchagua yeye,  hakikubaliki kwani kinawagawa Watanzania na kuwapa muelekeo wa kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa maadili,” ilisema taarifa ya NEC.

Ilifafanua kuwa: “ kifungu cha 2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015. “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya Udini, Ukabila, jinsia au rangi.”

Pia, NEC imevikumbusha vyama vya siasa kuzingatia kifungu cha 2.1(k) cha Maadili kinachoelekeza vyama au wagombea kutotumia majengo ya ibada kufanya kampeni na vyama au wagombea kutowatumia viongozi wa dini kupiga kampeni kwa ajili ya vyama vya siasa au wagombea wao.

Katika taarifa yake, NEC iliendelea kuonya kwa kusema kuwa: Lowassa na viongozi wengine wa CHADEMA wamekuwa na kauli za kuwaogofya wananchi kuwa ‘kura zitaibiwa’ na kwamba Tume itasababisha machafuko bila kutoa ufafanuzi jambo ambalo ni hatari.” 

Ilifafanua kuwa kauli hizo zinashangaza na kustaajabisha na ni kauli za hatari kipindi kama hiki,  kwa sababu kwa mujibu wa maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea, ambayo wagombea wote walipewa,  yana maelekezo kuhusu utaratibu mzima wa kupiga  na kuhesabu kura katika ngazi ya kituo, kujumlisha kura katika ngazi ya kata, jimbo na taifa.

NEC ilisema taratibu zote hizo hushuhudiwa na mawakala wa vyama vya siasa na wagombea ambapo kura zikihesabiwa ngazi ya kituo, mawakala hupewa nakala ya matokeo katika fomu Na. 21A kura za urais, 21 B kura za mbunge na 21 C kura za udiwani.

Katika ngazi ya jimbo, hesabu ya kura za kila kituo zilizopo pia katika nakala ya fomu 21A za urais na 21B za mbunge hujumlishwa na matokeo kujazwa katika fomu 24 A kwa Rais na 24B Mbunge na nakala ya matokeo wanapewa mawakala wa vyama na wagombea waliopo katika kituo cha kujumlishia kura ngazi ya jimbo.

“Katika ngazi ya taifa…hujumlisha matokeo ya kura za Rais mbele ya wagombea na mawakala wa vyama na kutangaza matokeo. Katika hali hii itabidi waeleze wizi unafanyika wapi,” ilihoji taarifa hiyo ya NEC.

Pia, NEC imekanusha madai ya kuegemea chama tawala ambayo yalitolewa na Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe na kuwa hali hiyo   itasababisha uvunjifu wa amani.

“Hili nalo ni tamshi lisilo la ukweli kabisa.Wakati wote Tume haiegemei wala kupendelea chama chochote katika kazi zake…Mbowe anajua hivyo Chaguzi zote Tume imefanya kwa kutegemea kura halali zote na ndiyo maana hata wabunge wa vyama vingine walitangazwa,” ilifafanua taarifa hiyo.

Ilishauri kuwa: Vyama vya siasa vijielekeze kwenye kutumia muda mwingi kuelezea, sera za vyama vyao ili ziweze kupimwa na wapiga kura badala ya kuchochea uhasama kati yao na serikali na Tume ya Uchaguzi.”

NEC ilionya kuwa haitasita kukifikisha chama au mgombea mbele ya Kamati ya Maadili ili aweze kuthibitisha kauli yake na anaposhindwa kamati itaweza kutoa adhabu kali kwa chama au mgombea husika ikiwa ni pamoja na kukatazwa kampeni kwa mhusika.

No comments:

Post a Comment