Monday 9 November 2015

SAMIA AWAONYA WATUMISHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS



Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, akitia saini kitabu baada ya kuripoti ofisini kwake jana

 
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais mstaafu Dk. Mohamed Gharib Bilal na baadhi ya wafanyakazi wa ofisi yake jana
NA MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka watumishi wa ofisi yake kufanyakazi kwa bidii na kwamba watakaopitwa na kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu’, wakae pembeni.
Samia alisema hayo jana, Ikulu mjini Dar es Salaam, baada ya kukabidhiwa ofisi na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Baada ya makabidhiano hayo, Samia alikaribishwa na watumishi wa ofisi yake, ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka kufanyakazi kwa bidii kulingana na kauli mbiu ya 'Hapa ni kazi tu'.
“Kila mmoja afanyekazi kwa bidii mahala pake pa kazi. Wale ambao kauli mbiu ya Hapa ni kazi tu itawapita, wakae pembeni, watatusamehe,” alisema Samia akiwaonya watumishi hao.
Aliwataka watumishi wa ofisi hiyo kupendana na kushirikiana ili kufanikisha azma ya kuleta matarajio ya maendeleo ya Watanzania, wanayotaka kuyaona katika uongozi wa awamu ya tano.
Makamu huyo wa rais, baada ya kutoa nasaha hizo, alifanya kikao na menejimenti ya ofisi, ambapo alitoa uelekeo wa utendaji kazi katika ofisi hiyo, hususan kuzingatia kusimamia masuala ya muungano na mazingira ili kufanikisha malengo ya serikali.
Samia aliitaka menejimenti hiyo kujipanga upya na kuacha kufanyakazi kwa mazoea kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwa upande wa masuala ya muungano na mazingira.

No comments:

Post a Comment