Wednesday 11 November 2015

MUHIMBILI HAKUKALIKI, VIGOGO WAJIFUNGIA VIKAONI KUJIPANGA UPYA





VIONGOZI na watendaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wameanza kujifungia ili kujipanga upya juu ya namna watakavyotekeleza majukumu yao na kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni kuhakikisha viongozi na wafanyakazi wanakwenda na kasi ya utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli na utekelezaji wa falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa vitendo.
Hayo yamekuja ikiwa ni siku moja baada ya Dk. Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza Hospitali ya Muhimbili, kujionea hali halisi ya utoaji huduma, ambapo alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya mambo aliyoyaona.
Katika ziara yake hiyo hospitalini hapo, Dk. Magufuli alivunja Bodi ya Muhimbili, ambayo ilishamaliza muda wake na kumng’oa Dk. Hussein Kidanto, aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MNH.
Aidha, alimteua Profesa Lawrence Mseru, kaimu nafasi hiyo kuanzia jana, hatua ambayo imewafurahisha Watanzania wengi, wakiwemo wagonjwa ambao baadhi walinyanyuka vitandani kumshuhudia. 
Jana, UHURU lilitembelea hospitalini hapo kujionea mambo yanavyokwenda ambapo, ilielezwa kuwa viongozi wa kada mbalimbali walikuwa wakiendelea na vikao kwa ajili ya kujipanga na kutekeleza maelekezo waliyopewa na Dk. Magufuli.
Aidha, wakati vigogo hospitalini hapo wakiendelea na vikao, wafanyakazi wa kada zingine walikuwa wakihaha huku na kule kutoa huduma kwa wagonjwa huku kila mmoja akiongeza bidii katika kutekeleza majukumu yake.
Hali ya utoaji wa huduma hospitalini hapo ilionekana kuwa tofauti na siku zingine zilizopita kabla ya Dk. Magufuli kufanya ziara hospitalini hapo, huku madaktari wakinyooshewa kidole kufanya kazi kwa muda mfupi na kukimbilia kwenye hospitali binafsi.
“Hapa kuna baadhi ya madaktari wanaondoka kabla ya wakati na kwenda kutoa huduma katika hospitali binafsi na kuwaacha wagonjwa wakiwa katika msururu mrefu wa kusubiri kuhudumiwa,” alidai mmoja wa wauguzi hospitalini hapo.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa wakipatiwa matibabu hospitalini hapo katika wodi za Mwaisela na Sewahaji, walisema ziara hiyo itasaidia kuokoa maisha ya baadhi yao kwa kuwa watahudumiwa haraka na kwa viwango vinavyostahili.
Walisema mgonjwa anaweza kulazwa kwa zaidi ya wiki mbili bila ya kupatiwa matibabu, kutokana na kuharibika kwa baadhi ya vipimo na kulazimika kwenda kupima katika hospitali binafsi kwa wenye uwezo.
Mgonjwa mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Chacha, alisema alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo muda mrefu, lakini alishindwa kutokana na kuharibika kwa kipimo cha CT-Scan.
Alisema baadhi ya wagonjwa wenye fedha wamekuwa wakifanyiwa baada ya kwenda kupima kipimo hicho katika hospitali binafsi, lakini alishindwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za vipimo.
Awatu Mbena, ambaye anamuuguza mtoto wake aliyelazwa hospitalini hapo, alisema ziara ya rais imeudhihirishia umma kwamba kwa sasa wananchi wote hata wa hali ya chini watahudumiwa vizuri.
Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa juzi jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ikimkariri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilisema rais alisikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini.
Pia, alikasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi, ambapo alikuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-Scan zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko. 
Balozi Sefue pia amesema, Rais Magufuli ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili, kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa, ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi ipasavyo.
Tayari Wizara ya Fedha imetoa sh. bilioni tatu kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote.
Balozi Sefue pia ametumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi, kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.

No comments:

Post a Comment