Thursday 15 December 2016

MPOGOLO AWATAKA WANA-CCM KUMPA USHIRIKIANO KUTATUA CHANGAMOTO




Na Bashir Nkoromo
 

Naibu Katibu Mkuu mpya wa CCM-Bara, Rodrick Mpogolo, amesema, anazitambua changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa Chama Cha Mapinduzi na kuahidi kushirikiana na wafanyakazi hao kuzipatia ufumbuzi.

Mpogolo amekutana na wafanyakazi hao ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, kilichofanyika jana, Ikulu jijini Dar es Salaam.

"Mimi nimekuwa katika chama hiki mda mrefu sana, kwa hiyo sehemu kubwa ya changamoto zinazowakabili wafanyakazi nazijua hivyo nitatumia juhudi zangu na maarifa kuhakikisha changamoto hizo zinapungua au kuisha kabisa".

"Lakini kubwa zaidi ni mimi na ninyi wafanyakazi kushirikiana kwa pamoja katika kupambana na changamoto hizi na hatimaye tukifikishe chama kunakotarajiwa, na bila shaka mnajua lengo kuu la Chama chochote ni kuwa na nguvu na inayokipa uwezo wa kuongoza kwa kushika dola", alisema Mpogolo.

Alisema, pamoja na kuwa katika Chama kwa mda wa kutosha kujifunza ana kuelewa mengi, lakini bado atahitaji ushauri kwa baadhi ya wafanyakazi wazoevu, hivyo wafanyakazi wasisite kumpa ushauri wao pale watakapokuwa wanaona kwamba ushauri wao utasaidia kusonga mbele.

Mpogolo aliwataka wafanyakazi kuongeza bidii ya kazi kila mmoja katika nafasi yake, akisema ni lazima watambue kuwa kila mfanyakazi wa Chama katika eneo aliloko mchango wake unahitajika sana, na aelewe kuwa isingekuwepo haya ya chama kumwajiri kama hakitarajii tija kutoka kwake.

Mapema, Mpogolo aliwasili ukumbini akifuatana na Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Rajab Luhwavi ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Balozi.

Luhwavi aliwaomba wafanyakazi kumpa ushirikiano Naibu Katibu Mkuu huyo mpya akimwelezea kuwa ni Kada wa Chama ambaye amefanya kazi katika idara nyingi na nyeti hivyo anayo hazina ya mambo mengi anayofahamu katika chama.


No comments:

Post a Comment