DIWANI wa Kata ya Siuyu, Tarafa ya
Mungaa, Jimbo la Singida Mashariki, Jared Justin (CHADEMA), amehukumiwa kwenda
jela miezi sita, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuzuia wakala wa kukusanya
mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Imedaiwa kuwa jimbo hilo pekee
mkoani Singida, ambalo lipo mikononi mwa upinzani (CHADEMA), lina sera ya
kuzuia wananchi wake kuchangia maendeleo kwa madai kuwa hilo ni jukumu la
serikali.
Mahakama ya Mwanzo ya Ikungi, chini
ya Hakimu Simon Kiyinga, ilimuhukumu diwani huyo kijana kwenda jela juzi, baada
ya kuridhishwa na upande wa Jamhuri.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Februari
13, mwaka huu, saa tatu asubuhi, katika mnada wa Njiapanda, mshitakiwa alimzuia
Ofisa Mwidhiniwa, Amina Abdallah wa Kampuni ya Abada Care Investment, kufanyakazi
ya kukusanya ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Kwa mujibu wa hati ya upande wa
mashitaka, siku ya tukio, mshitakiwa alitenda makosa mawili, ikiwa ni pamoja na kumuzuia Amina kufanyakazi
yake ya kukusanya mapato ya halmashauri, kitendo ambacho ni kinyume na kifungu
cha 12 (e), sheria ndogo ya Halmashauri ya Ikungi.
Aidha, mshitakiwa pia alituhumiwa
kutenda kosa la kushawishi wananchi waache kuchangia mapato kwa halmashauri yao,
kinyume na sheria ndogo kifungu cha 12 (1) (c).
Hata hivyo, Hakimu Simon Kiyinga
alitupilia mbali tuhuma za kosa la pili kwa kuwa ushahidi uliotolewa hautoshi kumtia
hatiani mshitakiwa.
Hakimu Kayinga alisema kwa kosa la
kwanza la kumuzuia ofisa kukusanya mapato yaliyobainishwa na Halmashauri ya
wilaya ya Ikungi, ushahidi wa upande wa mlalamikaji, umethibitisha bila kuacha
shaka yoyote kwamba ana hatia kama alivyoshitakiwa.
Kwa hali hiyo, alisema mshitakiwa
atakwenda jela miezi sita, ili iwe fundisho kwake na kwa madiwani wengine
wanaotarajia kufanya kosa kama hilo.
No comments:
Post a Comment