Wednesday 23 March 2016

MAJALIWA ATOA MAAGIZO SOKO LA FERI





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, kukutana na kampuni mbalimbali zinazouza gesi ili kupata inayouza kwa bei nafuu zaidi, lengo likiwa kuwapunguzia gharama  wakaangaji wa samaki sokoni hapo.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amemtaka Meneja wa soko hilo, Solomon Mushi, kuhakikisha wanakuwa na kifaa maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi ya gesi sokoni hapo ili kubaini kama ni sahihi.

Alitoa agizo hilo jana, wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo, ambapo aliridhishwa na unavyofanya kazi.

Waziri Mkuu, ambaye alitumia dakika 44, kulitembea soko hilo, alitoa maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara, ambao wamesema wamekuwa wakiuziwa gesi kwa bei kubwa na imekuwa ikiongezeka mara kwa mara.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Ally Iddi, alisema awali walikuwa wanauziwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32, kwa sh. 70,000, lakini sasa umeongezeka hadi sh. 98,000, kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na uzalishaji wao.

“Nimeulizia kwenye baadhi ya maduka na kukuta mtungi wenye ujazo kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.

Kijana mwingine, ambaye ni mkaangaji wa samaki, Mwanya Selemeni, alisema hivi sasa hali ya soko la feri ni nzuri, tofauti na walivyokuwa wakitumia kuni kwa sababu hakuna moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe wanafikishiwa gesi ya kutoka Mtwara ili gharama ziweze kupungua.

Naye Mariam Samweli, alimuomba Waziri Mkuu wapatiwe umeme kwenye mabanda yao ili watafute biashara zingine za kufanya.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alitembelea eneo la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo, ambako alielezwa matatizo ya umeme na uzibaji wa mitaro ya maji machafu, hali ambayo inatishia usalama wa afya zao.

“Kuna jipu la umeme hapa, tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye hatumjui, lakini hatujawahi kuona risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu na umeme wenyewe wala haukai. Mita tunayo hapa, lakini hata namba hatujapewa,” alisema Omari Masoud kwa niaba ya wenzake.

Kuhusu tatizo la uzibaji mitaro na kutiririsha majitaka, kiongozi wa mama lishe sokoni hapo, Fatma Ally, aliomba watatuliwe tatizo hilo, ambalo limedumu kwa zaidi miezi miwili.

Akijibu kero hizo, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, asimamie suala la kuweka umeme kwenye banda na kuhakikisha mama lishe wa soko hilo upande wa mnadani, waanze kutumia majiko ya gesi badala ya mkaa.

Kuhusu mitaro, alimwagiza meneja wa soko hilo,  Solomon Mushi aimarishe uzibuaji wa mitaro.

“Mwambie mkandarasi azibue mitaro kila siku jioni na watumiaji wa soko waache kutumia mifuko ya plastiki kwa sababu inapoingia kule, inaziba na wala haiozi,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya chakula. “Lengo letu ni kufanya soko hili liwe kwenye viwango vya kimataiafa ili mteja anapokuja kununua samaki wabichi ama wa kukaanga, awe na chaguo,” alisema.

Kwa upande wake, Mushi alisema bodi ya soko hilo, ambayo imeundwa hivi karibuni, itakutana kesho kwa mara ya kwanza na miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART), yataanza kufanyiwa majaribio ndani ya wiki moja kuanzia sasa, ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.

“Wataanza na mabasi kati ya 30 – 50, ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine, wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.

Alitoa kauli hiyo jana, wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.

Waziri Mkuu, ambaye alitembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa jibu hilo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara, Sharifu Ramadhani, ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja.

“Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taksi ni gharama kubwa,” alisema.

Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema: “Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi, ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki, ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”

Alisema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza kazi.

No comments:

Post a Comment