Saturday, 27 August 2016

WABUNGE WA CUF WADAIWA KUGOMEA UKUTA, DK. MWAKYEMBE ATOA ONYO KALI

WABUNGE kutoka Chama cha Civil United Front (CUF) Zanzibar, wamesema hawatashiriki maandamano ya UKUTA kwa kuwa wao si wanachama wa CHADEMA, huku wakiweka bayana uamuzi wa kukurupuka wa kuingia kwenye  UKAWA ndio umesababisha chama hicho kusambaratika.

Pia, wabunge hao wamezikataa fulana zenye maneno ya uchochezi ya UKUTA kwa kuwa maandamano hayo hayana maslahi kwa chama chao na wananchi.

Aidha, wamesisitiza kuwa hawako tayari kukubali kuona chama hicho kinaridhia matakwa ya baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kutoka Tanzania Bara, wanaotaka kurejeshwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambapo walieleza kuwa wajumbe hao wamepandikizwa na CHADEMA ili kuzidi kukidhoofisha chama hicho.

Kauli za wabunge hao, wamezitoa wakati chama hicho kikiwa kwenye mpasuko uliojitokeza dhahiri Agosti 21, mwaka huu, wakati wajumbe wa mkutano mkuu waliporushiana makonde kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, baada ya kuibuka kwa hoja ya kutaka kujadiliwa barua ya Profesa Lipumba ya kujiuzulu uenyekiti.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina, wabunge hao walisema hawaoni umuhimu wa chama hicho kuendelea na UKAWA kwa kuwa unaendeshwa kwa maamuzi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, na amekuwa akifanya maamuzi yasiyokuwa na tija kitaifa na kisiasa.

Walisema uamuzi wa kukurupuka uliochukuliwa na CUF kujiunga UKAWA, ulikisababishia chama hicho kuwa kwenye hali ngumu kifedha, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

"Hawa ndio waliomshawishi Maalim Seif (Katibu Mkuu wa CUF), kugomea kushiriki marudio ya uchaguzi, matokeo yake tumepoteza majimbo yote kwenye baraza la uwakilishi, UKAWA ulikuwa ni mkakati wa kutumaliza kisiasa.

"Wamesababisha tukose fedha, leo wanatuburuza tukaandamane, huo UKUTA  una manufaa gani kwetu, wakati tunaishi katika maisha magumu wao wanajinufaisha," alisisitiza mmoja wa wabunge hao.

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa vikao vya kamati za bunge vinavyoendelea mjini Dodoma, wabunge kwa pamoja waliazimia kutochukua na kuvaa fulana za maandamano ya UKUTA kwa kuwa hazina umuhimu.

Walisisitiza kuwa kuvaa fulana za UKUTA ni kitendo kitakachotafsiriwa kama nidhamu ya uoga na kitazidi kukisambaratisha chama chao.

WAMPIGIA GOTI JPM

Wakati hayo yakijiri, viongozi wa UKUTA wamewaomba viongozi wa dini kuwaunganisha na Rais Dk. John Magufuli ili kukaa meza moja kwa ajili ya kumaliza utata wa masuala ya kisiasa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam.

Mbatia alisema kutokana na Tanzania kuwa ni nchi ya amani na inasuluhisha migogoro mingi barani Afrika, ni jambo la busara wakakaa meza moja na Rais Magufuli kwa ajili ya mazungumzo.

“Kwa mfano, Rais mstaafu Benjamin Mkapa alikuwa akimpigia debe Rais Dk.  Magufuli na pia ni msuluhishi wa migogoro barani Afrika na hivi ninavyozungumza yupo Burundi kwa ajili ya usuluhishi, kwa nini na hili lisitatuliwe?” Alihoji.

Alisema duniani kote sasa hivi migogoro yote huwa inasuluhishwa na meza ya mazungumzo ya pamoja kwani ndiyo njia pekee ya kutatua migogoro.

“Tutumie busara na hekima katika kumaliza hili,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi wa dini kuingilia kati suala hilo ili liweze kumalizika kwa amani bila mgogoro wowote.

Katika hatua nyingine, wabunge wa vyama vya upinzani wameshauriwa kurudi bungeni kwa ajili ya kutetea maslani ya Watanzania.

Ushauri huo ulitolewa juzi, walipokutana na viongozi wa dini nchini kwa ajili ya kuzungumzia masuala mbalimbali.

Mbatia alisema walikutana na viongozi hao kwa ajili ya kuzungumzia mustakabali mzima wa taifa na Watanzania kwa ujumla.

Aidha, alisema kubwa walilolizungumzia ni kushauriwa kurudi bungeni kwa ajili ya kupigania maslahi ya wapiga kura wao.

Alisema ushauri huo wa kurudi bungeni, wameupokea na wataufanyia kazi ili bunge linaloanza Septemba 6, mwaka huu, waingie kwa ajili ya kuwawakilisha wapiga kura wao.

“Viongozi wa dini wametupa ushauri mzuri sana, ambao tumeupokea na tutaufanyia kazi ili bunge lijalo tuingie kwa ajili ya kutetea maslahi ya wapiga kura wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema.

Kwa upande mwingine, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa ACT-Mzalendo, Addo Shaibu, alisema hawawezi kushiriki kwenye maandamano hayo kwa sababu hawakupata barua ya mwaliko kutoka CHADEMA.

MWAKYEMBE: ZINGATIENI AMRI HALALI YA POLISI

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema amri ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya nje na ndani ya vyama vya siasa ni halali, ambayo kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote cha siasa, anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Amesema amri hiyo ni ya kudumu, ambayo imelenga kuangalia na kufanya tathmini ya hali ya nchi kutokana na viashiria mbalimbali vya uvunjifu wa amani nchini, ambavyo vimeanza kuonekana.

Dk. Mwakyembe alikuwa akijibu swali kutoka kwa Kituo cha Televisheni cha Taifa TBC 1, ambalo lilitaka kupata ufafanuzi kuhusiana na uhalali wa kauli ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.

“Jeshi  la Polisi ni chombo halali cha dola kilichoanzishwa kisheria, chenye wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema Mwakyembe.

Aliongeza kuwa uamuzi huo una lengo la kulinda amani ya nchi na endapo kutakuwa na viashiria vya kutishia amani ya nchi, lazima hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe.

"Ni amri halali na kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote nchini anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba, kwenda kinyume ni kukiuka sheria,” alisisitiza Dk. Mwakyembe.

Alisema ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano, lakini wanatakiwa kutoa taarifa polisi ili waweze kutoa ulinzi wakati wa mkutano huo na kuongeza kuwa, Jeshi la Polisi linaweza kuzuia mikutano hiyo kwa sababu za kiusalama.

Waziri Mwakyembe pia alisema sio kweli kuwa rais amezuia mikutano ya siasa, bali alichofanya ni kudhibiti uendeshaji holela au huria wa shughuli za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya wanasiasa na kuongeza kuwa,  Rais Magufuli amefanya hivyo kutokana na kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taifa kwa ujumla.

“Rais hajapiga marufuku siasa, alichofanya ni kudhibiti uendeshaji holela au huria wa shughuli za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya wanasiasa husika ili kuepusha shari na chuki na amefanya hivyo kutokana na kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Tanzania na taifa kwa ujumla  wake.

"Kwa hatua hiyo, rais hajafunga milango ya majadiliano, milango iko wazi na tulitegemea wenzetu wangekuja na njia mbadala na kulizungumzia hilo badala ya kuitisha maandamano ya nchi nzima", alisema.

Dk. Mwakyembe amevitaka vyama vya upinzani nchini kukaa na kuzungumza na serikali na kuacha kufanya vitendo vya kutishia uvunjifu wa amani kama kuitisha maandamano kwa nchi nzima.

“Njooni tukae tuzungumze tupime ushauri wenu, hili ni taifa letu, tena milango iko wazi, tuache kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani kama ambavyo inavyoonekana nchini hivi sasa,”alisisitiza.

Alifafanua kuwa, Sheria ya Vyama vya Siasa hairuhusu kufanyika kwa maandamano kwa nchi nzima, kufanya hivyo ni kuchochea wananchi kuasi 'civil disobedience' na ni kinyume cha sheria na serikali haiwezi kuivumilia hali hiyo.

Waziri Mwakyembe alitoa wito kwa Watanzania wote kutoshiriki maandamano ya UKUTA, ambayo alisema hayatakuwa na tija kwa nchi bali kuleta vurugu katika jamii.

MAANDAMANO MARUFUKU TANGA

Serikali wilayani  Tanga imesema imejipanga kikamilifu kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA, huku ikiwataka kusitisha maandamano yao kabla hatua nyingine za kuwadhibiti hazijachukuliwa.

Hata hivyo, imesema zipo taarifa za kuwepo vikundi vinavyoandaa na kutekeleza mpango wa maandamano yaliyoandaliwa na chama hicho, yatakayofanyika Septemba Mosi, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, alisema  anazo taarifa za ujio wa wabunge wanne wa chama hicho watakaofika jijini Tanga leo, kwa ajili ya kuandaa na kuwashawishi wananchi washiriki maandamano hayo yaliyopigwa marufuku na serikali.

Mwilapwa alisema wanazo taarifa kuhusu ujio wa wabunge (hakuwataja majina), mahali watakapolala na watu watakaowapokea  na kushirikiana kuhusu maandalizi ya mpango huo.

“Tanga hatufanyi masihara, tunazo taarifa, wapo wabunge wanne watakuja kesho (leo) kufanya maandalizi, majina yao tunayo na nani anafanya maandalizi watakapokuja, watakaoshirikiana nao na mahala watapolala tunajua,” alisema Mwilapwa akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Aidha, alisema wabunge hao watakapofika mkoani hapo kazi yao kubwa itakuwa ni kuhamasisha watu waandamane na kufanya fujo na endapo wananchi wa Tanga kutokana na utulivu wao watakataa, wamepanga kufanya mkutano.

Mkuu huyo wa wilaya aliwahadharisha viongozi wa vyama vya siasa kutumia utaratibu sahihi katika kujenga demokrasia, badala ya kuleta vurugu, fujo na kufanya matukio yasiyoendana na sheria zilizopo nchini.

Mwilapwa alisema kitendo cha waandaji wa mpango huo lolote likitokea kabla na baada ya mpango huo, serikali itawashukia hasa ikizingatiwa Jiji la Tanga huko nyuma, lilikuwa katika vita kubwa ya kupambana na majambazi katika eneo la Amboni, hivyo kufanya kwao fujo kunakumbushia matukio hayo.

No comments:

Post a Comment