Saturday, 27 August 2016

JWTZ YAJIPANGA KUADHIMISHA SIKU YA MAJESHI

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetangaza kufanyika kwa maadhimisho ya Sikukuu ya Majeshi, Septemba Mosi, mwaka huu.

Maadhimisho hayo yatafanyika kupima mafanikio yaliyofikiwa na jeshi hilo tangu lilipoanzishwa Septemba Mosi, mwaka 1964, kwa kushirikiana na wananchi kwa kuwa JWTZ jukumu lake ni kuwalinda wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga, alisma maadhimisho hayo yatafanyika sanjari na utoaji wa huduma mbalimbali za afya pamoja na kushiriki usafi kwenye maeneo mbalimbali.

Alisema wanajeshi watajitolea damu kwenye hospitali za jeshi za Lugalo, Mwanza, Mirambo mkoani Tabora, Bububu iliyoko Zanzibar, Mazao KJ iliyoko Morogoro, Arusha (TMA) pamoja na hospitali ya 411 SVC Luhwiko iliyoko Songea.

Aliongeza kuwa madaktari wa JWTZ, watatoa huduma za tiba bure, ushauri nasaha, upimaji virusi vya ukimwi (VVU), kisukari pamoja na upimaji wa shinikizo la damu.

“Pia, madaktari wetu watashirikiana na kanda zote za Damu Salama Tanzania, kuchangia damu kwenye matawi kwa ajili ya hospitali za umma.

“Lakini kama ilivyo mila na desturi za majeshi mbalimbali duniani, jeshi litafanya usafi sio kwenye kambi pekee, bali hata nje ya kambi za jeshi,” alisisitiza Kanali Lubinga.

Alieleza kuwa JWTZ litafanya usafi pamoja na upandaji miti kwenye maeneo jirani na kambi zake na taasisi za kiraia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya serikali, inayosisitiza utunzaji wa mazingira ili kuepukana na magonjwa.

Jeshi hilo limewaomba wananchi kujitokeza kupata huduma mbalimbali za kiafya.

Akizungumzia kuhusu maandamano ya UKUTA, yaliyopangwa kufanywa kundi la wanasiasa, msemaji huyo wa jeshi, alisema tayari taasisi husika za kiserikali zimeshatolea tamko, hivyo jeshi litafanya maadhimisho hayo kama ilivyopangwa.

No comments:

Post a Comment