WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, George Simbachawene ameanika mageuzi makubwa yanayoendelea mikoani katika utekelezaji wa ahadi za serikali ya awamu ya tano, huku akisisitiza hii ni awamu ya kazi tu na sio maandamano yasiyo na tija.
Waziri Simbachawene aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, jana, katika kipindi kipya cha televisheni kiitwacho 'TUNATEKELEZA', kinachorushwa na TBC1.
Katika mahojiano hayo maalumu, Simbachawene alisisitiza kuwa, Rais Dk. John Magufuli anaamini katika maendeleo ya wananchi na sio siasa, hivyo amewataka wananchi na wadau wengine wajipange kwa mwelekeo huo.
“Nimeshukuru hata kipindi hiki mmekiita TUNATEKELEZA, kwa sababu Mheshimiwa Rais na serikali kwa ujumla, tumedhamiria kwa dhati kuifikia Dira ya Taifa, kwa kutekeleza ahadi tulizozitoa kwa wananchi,” alisema.
Akizungumzia utekelezaji unaoendelea, Simbachawene alisema kuna mageuzi makubwa yanayotokea mikoani kwa sababu kwa sasa, kila mtendaji wa serikali anajua kuwa, hana namna nyingine zaidi ya kuwajibika na kuwaletea maendeleo wananchi.
“Utaona kwamba wizara yangu hii, ambayo kimsingi ndio kiungo cha huduma zote zinazotekelezwa kwa wananchi, kwa sasa imeongeza ufanisi sana katika usimamizi na ubora wa miradi inayotekelezwa,” alisema.
Akitoa mfano kuhusu sera ya elimu bure, Waziri Simbachawene alisema sera hiyo imewasaidia wananchi wengi maskini waliokuwa wakishindwa kuwasomesha watoto wao kwa kukosa uwezo.
Hata hivyo, aliwaonya walimu wakuu na wasimamizi wengine wa elimu kuwa, atakayejaribu kucheza na fedha hizo zitamtokea puani.
Aliongeza kuwa wizara yake pia imehakikisha halmashauri nyingi zinakusanya mapato kwa kiwango cha juu, ambapo alisema hivi sasa halmashauri nyingi zimeongeza ukusanyaji huo na pia nidhamu ya watendaji imeongezeka.
“Kuna sehemu watu walikuwa wanakusanya laki tatu tu. Leo ninavyokwambia, wanakusanya mpaka milioni tano. Hii itasaidia kutujengea zaidi uwezo wa kujitegemea,” alisema.
Moja ya mafanikio ya wizara yake na uongozi wa Rais Magufuli kwa ujumla, alisema ni kupambana ipasavyo na changamoto ya wafanyakazi hewa.
Akizungumzia hilo, alisema tayari wafanyakazi hewa zaidi ya 12,000, wamebainika na kuondolewa kwenye mfumo wa malipo. Alisema wafanyakazi hao hewa, wapo waliokuwa madaktari, manesi, walimu na watu wa fani nyingine.
“Tumepambana kwa kiasi kikubwa na suala la wafanyakazi hewa na hii itasaidia sasa tuweze kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. Wengi zaidi wataondoka kutokana na hili zoezi la ukaguzi wa vyeti linaloendelea,” alisema.
Waziri Simbachawene alisema anaamini dira na maono ya Rais Magufuli, vimebeba nia njema kwa wananchi na kuonya kuwa, kwa sababu hiyo serikali haitaruhusu siasa zikwamishe maendeleo na kufikiwa kwa maono hayo.
Kuna watu wanakuja na maneno ya udikteta. Hivi udikteta ndio huku kuwabana wabadhirifu? Au ndio huku kuwabana watu wafanye kazi? Au ndio huku kuhakikisha miradi inatekelezwa vyema? Sisi tuko kazini, hivyo hatutaruhusu mtu atuzuie kutekeleza Ilani yenu kwa kudai eti anaandamana. Hapana.”
Kipindi hicho kipya, kitahusisha mawaziri kuainisha kwa umma utekelezaji wa mara kwa mara wa majukumu waliyopewa na Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment