Saturday, 27 August 2016

MAALIM SEIF APEWA SIKU SABA KUJIELEZA

SINTOFAHAMU imezidi kuibuka ndani ya chama cha Civic United Front (CUF), baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumpa siku saba Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, atoe sababu za kuvunjika kwa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho.

Pia, ofisi hiyo imesema endapo akishindwa kutoa maelezo kwa siku hizo, atakwenda jela kwa kipindi cha miezi sita au kutoa faini ya sh. 30,000 au kutumikia vyote kwa pamoja.

Uamuzi wa msajili ulifikiwa juzi, baada ya wajumbe zaidi ya 324, kuandika barua ya malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kueleza ubabe na kupindishwa kwa sheria katika mkutano huo.

Mkutano huo uliofanyika Jumapili ya wiki iliopita kwenye ukumbi wa Blue Pearl, ulioko Ubungo, jijini Dar es Salaam, ulivunjika baada ya wajumbe kutoridhika na mambo yalivyokuwa yakiendeshwa na Maalim Seif.

Mwenyekiti wa mkutano huo, Julius Mtatiro, alidai kuwa wajumbe wameafiki uamuzi wa kukubali barua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Profesa Ibrahimu Lipumba.

Jambo hilo lilionekana kuzusha sintofahamu kubwa miongoni mwa wajumbe, ambao hawakukubaliana na uamuzi huo kwa madai taratibu nyingi zilikiukwa, ikiwemo kuwepo kwa wajumbe feki kwenye kikao hicho.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe 324 wa mkutano huo waliandika barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kueleza masikitiko yao na msajili kuijibu barua hiyo, kupitia kwa Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza.

Katika barua hiyo, CUF inapaswa ijieleze sababu za kuvunjika kwa mkutano huo kwa kuwa wajumbe wamefikisha malalamiko yao.

Barua ya msajili kwenda CUF, yenye kumbukumbu namba NK.322/362/14/40, imemtaka Katibu Mkuu kueleza sababu za kuvunjika kwa mkutano huo.

Pia, msajili amesema amechukua uamuzi huo kwa kufuata sheria na kanuni za vyama vya siasa.

Msajili alisema kanuni hizo zinampa haki msajili kuomba kupewa maelezo yeyote kutoka kwa ofisa wa chama na msajili anapaswa kujibiwa kama alivyoagiza.

Gazeti hili lilipofika makao makuu ya CUF eneo la Buguruni, lilishindwa kupata ushirikiano baada ya wafuasi wa chama hicho kumzuia mwandishi.

No comments:

Post a Comment