Saturday, 27 August 2016
WALIOFURAHIA MAUAJI YA ASKARI KWENYE MITANDAO KUKIONA CHA MOTO
VILIO, simanzi na huzuni vilitawala jana, Polisi Baracks, Kilwa Road, wakati wa kuagwa kwa miili ya askari wanne waliouawa na majambazi, wakati wakibadilishana lindo, maeneo ya Mbagala Mbande, Dar es Salaam.
Wakati wa kuugwa kwa askari hao, viongozi mbalimbali wa serikali na Jeshi la Polisi walihudhuria, ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwingulu Nchemba, alitoa maagizo mazito likiwemo la kushughulikiwa wale wote waliokuwa wakituma ujumbe wa kejeli huku wakifurahia mauaji hayo kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema inastahili familia za askari wanaokufa katika mapambano, kujengewa nyumba ili iwe kumbukumbu kwao.
“Ni jambo baya ambalo tutapambana hadi tuwapate. Vijana wetu wamekufa wakipambana. Sisi kama wizara, tumeguswa sana kwa kuwa walikuwa hawajafanya kosa na siku hiyo walikuwa wameshamaliza kazi yao.
“Tutapambana na waovu hadi mwisho. Vijana wetu walikuwa kazini katika taasisi ya kifedha, kwani wanajitolea kuwa mstari wa mbele kutulinda wakati tukiwa tumelala,” alisema Waziri Nchemba.
Aliongeza kuwa baadhi ya watu waliandika kwa kejeli huku wakifurahia mauaji hayo, hivyo serikali haiwezi kuwafumbia macho, lazima ijue lengo lao.
“Lazima tujue lengo lao, lazima tuwashughulikie kwa kuwa wale waliofanya hivyo wamejitangaza kwamba wanashiriki tukio hilo moja kwa moja,” alisema.
Waziri huyo alisema watu hao lazima wachukuliwe hatua stahiki ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
Aidha, Waziri Nchemba alisema wataangalia utaratibu wa huduma za bima kwa familia za askari wanaokumbwa na majanga kama hayo ili familia zao zisitetereke.
JPM ATOA RAMBILIRAMBI
Naibu Kamishna wa Polisi, Hezron Gimbi, alitoa salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Dk. John Magufuli, ambapo alisema ametoa sh. milioni 10, za rambirambi kwa familia za askari hao wanne.
Alisema yeye binafsi ameguswa na tukio hilo na kwamba, watu wengi wamekuwa hawapendi askari wawepo hapa nchini ndio maana wanafanya mauaji.
“Tukio hili limetupa nguvu ya kupambana zaidi na kuhakikisha wahusika wote tunawatia mbaroni,” alisema Kamishna Gimbi.
Alisema watahakikisha wanatekeleza agizo la waziri kwa kuwatia mbaroni wale wote wanaoshabikia tukio hilo.
Mbali na hayo, serikali imesema itatoa fidia ya sh. milioni 15 kwa askari hao wote.
Pia, uongozi wa Benki ya CRDB, ulisema utatoa rambirambi ya sh. milioni mbili, kwa kila familia ya askari hao na askari aliyeacha watoto watatu, watawapa bima ya mwaka mzima.
Meneja Mkuu wa Benki ya CRDB, Sebastian Masaki, alisema benki hiyo itatoa sh. milioni 10, kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha Polisi wilayani Temeke.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema askari wao wamepigwa risasi nyingi wakiwa kazini kwani wamekufa kishujaa huku wakiwa wanapigania usalama wa raia na mali zao.
"Wenzetu wamekufa na wale walioshiriki kuwaua wamewasha moto na sisi lazima tutajibu mapigo. Tutahakikisha tunasimama pande zote kwani tunatakiwa kuwaombea waliotangulia kwa kupigania haki,’’alisema Kamanda Sirro.
Kwa upande wake, Makonda alimuagiza Kamishna Sirro, kuhakikisha wanapopambana na majambazi walioko misituni, wawauwe kabisa na watu wa haki za binadamu wamfuate yeye kumuuliza.
Makonda alisema atashangaa kuona haki za binadamu kukaa kimya, bila ya kufanya maandamano kupinga mauaji ya askari hao wanne.
Alisema askari anayekufa katika mapambano, familia yake inastahili kujengewa nyumba ili iwe kumbukumbu.
Makonda alisema ni jambo la kushangaza kuona walinzi wa amani nchi hii, wanaowalinda wananchi wenzao na mali zao wanauawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, alisema tangu juzi, wamefanya uchangiaji kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikuu cha polisi katika wilaya ya Temeke.
Askari waliopigwa risasi juzi ni askari namba E.5761CPL Koplo Yahaya Malima, ambaye ameacha mke na watoto watatu, F. 4660CPL Hatibu, G.9524 Tito na G.9996 PC Gastone.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment