CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Rais Mteule wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kwa kupata ushindi wa kishindo katika
uchaguzi mkuu uliofanyika Machi 20, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha,
alimtangaza Dk. Shein kuwa Rais Mteule wa Zanzibar, baada ya kupata kura
299,982, sawa na asilimia 91.4, kati ya kura 341,865 zilizopigwa.
Katika uchaguzi huo wa marudio, uliokuwa wa amani na
utulivu, idadi ya wapiga ilikuwa 503,580 na kura zilizoharibika ni 13,327.
Jumla ya vyama 14 vilishiriki.
Akizungumza katika Ofisi Mkuu ya CCM Kisiwandui, mjini
hapa jana, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi, Waride
Bakari Jabu, alisema Dk. Shein, amepata ushindi wa kihistoria, ambao haukuwahi
kutokea katika historia ya demokrasia ya vyama vingi kwa upande wa Zanzibar.
Waride, alisema ushindi wa Dk. Shein umedhihirisha kuwa wananchi
wa Zanzibar wana imani kubwa na CCM kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya
Chama.
Pia, alisema CCM inampongeza Dk. Shein kwa kutoa hotuba
nzuri katika hafla ya kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, iliyofanyika Machi 21,
mwaka huu, katika ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani.
Katika hotuba hiyo, Dk. Shein, aliwaahidi wananchi wa
Zanzibar kuendeleza amani na utulivu wa taifa katika kipindi chote atakapokuwa
madarakani kwa miaka mitano.
"Mheshimiwa Rais Mteule Dk. Shein alielezea nia
yake ya kusimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015-2020 na kuinua hali ya kiuchumi kutoka asilimia saba hadi kufikia
10,"alisema Waride.
Katibu huyo alisema ushindi wa Dk. Shein umetokana na
juhudi na ushirikiano baina ya viongozi na wanachama wa CCM na Jumuia zake kwa ngazi zote za Unguja na
Pemba.
Aidha, aliwapongeza wanachama wa CCM na wananchi wa
Unguja na Pemba, kwa kutumia kikamilifu haki yao ya kidemokrasia kufanya uamuzi
stahiki wa kuichagua CCM na kumpa kura za kishindo Dk. Shein.
Waride, aliwapongeza viongozi, watendaji na wanachama wa
CCM ngazi zote na wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio.
Pia, Waride alitoa pongezi kwa vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kusimamia kwa umakini ulinzi katika mikoa yote ya Zanzibar na kuhakikisha
uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.
Mbali na Dk. Shein, wagombea wengine wa urais
waliopigiwa kura ni Khamisi Idd Lila wa Chama cha ACT-Wazalendo aliyepata kura
1,225, Juma Ali Khatib ADA-TADEA (1,562), Hamad Rashid Mohammed ADC (9,734).
Pia walikuwemo Said Soud Said wa AFP (1,303), Ali Khatib
Ali wa CCK (1,980), Mohammed Masoud Rashid wa CHAUMMA (493), Seif Sharif Hamad wa
CUF (6,076) na Tabu Mussa Juma wa D-MAKINI (210).
Wengine ni Abdallah Kombo Khamis wa DP (512), Kassim
Bakari Ali wa Jahazi Asilia (1,470), Seif Ali Idd wa NRA (266), Issa Mohammed
Zonga wa SAU (2,018) na Hafidh Hassan Suleiman wa TLP aliyepata kura 1,496.
Uchaguzi mkuu wa marudio ulifanyika Machi 20, mwaka huu,
baada ya ZEC kufuta uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, mji wa Unguja na vitongoji vyake juzi, ulilipuka kwa shangwe na nderemo kutoka kwa wanachama na mashabiki wa CCM na wengine kukesha wakishangilia ushindi wa Rais Mteule Dk. Shein.
Muda mfupi baada ya Dk. Shein kutangazwa Rais Mteule wa
Zanzibar, wanachama na mashabiki wa CCM waliingia katika mitaa mbalimbali
kufurahia ushindi huo, wakiwa na sare za rangi ya kijani na njano.
Katika ngome maarufu ya CCM, Maskani ya Kisonge, wanachama na mashabiki wa Chama walijitokeza kwa wingi kusherehekea ushindi huo.
Pia, magari yaliyofungwa bendera za CCM yalionekana
yakiranda mitaani kwa mbwembwe, huku nyimbo za kumsifu Dk. Shein na Rais Dk.
John Magufuli, zikichezwa.
Baadhi ya mabango yaliyobandikwa katika magari ya watu binafsi na vyombo vya usafiri yalisomeka: "Dk. Shein ndiye Rais wa Zanzibar, wapinzani hamna chenu, mpeni ushirikiano tuijenge nchi yetu."
Licha ya mbwembwe hizo, hali ilikuwa shwari katika mitaa mbalimbali ya mjini hapa, zikiwemo ngome za CUF Bububu, Darajani na baadhi ya vitongoji vya Mwanakwerekwe, Fumba na Maungani.
Ulinzi mkali uliimarishwa katika maeneo yote ya mji wa Unguja na wananchi waliendelea na shughuli kama kawaida na magari ya kusafirisha abiria (daladala) yalikuwa mengi, tofauti na Jumapili iliyokuwa siku ya kupiga kura.
No comments:
Post a Comment