Wednesday 23 March 2016

LUKUVI AIBANA NHC KWA KUPANDISHA KODI HOLELA




SERIKALI imelipiga marufuku Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kupandisha kodi za nyumba zake bila idhini ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Aidha, imelitaka shirika hilo kutoanzisha miradi mipya mikubwa hadi iliyoko ikamilike kwa muda uliopangwa na kwamba, lijenge nyumba kwa gharama nafuu.
Mbali na hilo, imelitaka shirika hilo kuendelea na muundo wake wa sasa na kuacha ule waliotaka kuuanzisha.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema hayo jana, makao makuu ya NHC, mjini Dar es Salaam, alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa bodi na menejimenti ya shirika hilo.
Alisema kuanzia sasa ni marufuku kwa shirika hilo kupandisha kodi za nyumba zake hadi wamtaarifu na waeleze sababu za kufanya hivyo.
Lukuvi aliitaka bodi kuunda kamati ndogo, ambayo itakuwa inashughulikia rufani za wapangaji wanaolalamikia ongezeko la kodi.
“Wapangaji wengi wanalalamikia kodi zenu, hivyo ni marufuku kupandisha kodi bila ya kunitaarifu na mnieleze kwa nini mnapandisha,” alisema.
Alisema lengo la serikali ni kuzipangisha nyumba za shirika hilo kwa wananchi wa hali ya chini na kwa bei inayoendana na uhalisia wa maisha yao.
Kuhusu miradi mipya, Lukuvi alilitaka shirika hilo kutoanzisha miradi mipya hadi iliyopo ikamilike.
“Nataka miradi mikubwa yote mliyonayo hakikisheni inakamilika kwa wakati uliopangwa na hakuna kuanzisha miradi mipya kabla ile ya zamani haijakamilika,” alisema.
Alilitaka shirika hilo kuhakikisha kuwa miradi mipya inayojengwa kwenye viwanja vilivyovunjwa nyumba za serikali, ardhi ya nyumba hizo ibaki kuwa mali ya serikali.
“Hakikisheni kila mnapojenga nyumba eneo la serikali, basi shirika liwe na hisa,” alisema.
Akizungumzia muundo wa shirika hilo, Lukuvi alisema uliopo unatosha na hakuna haja ya kuanzisha muundo mpya.
Lukuvi alisema ni vyema muundo uliopo ukaimarishwa badala ya kuunda mpya na kwamba, ni vyema menejimenti, bodi na wafanyakazi wengine wakaendeleza ushirikiano ulipo katika utendaji wao.
Hata hivyo, alitoa mwezi mmoja kwa bodi ya shirika hilo, kumpelekea mkakati wa namna watakavyotekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kujenga nyumba 50,000.
Alilitaka shirika hilo kuhakikisha linajenga nyumba za gharama nafuu zinazolingana na maisha ya kawaida ya Mtanzania.
“Mnapojenga nyumba za gharama nafuu, basi msihitaji faida kubwa kwenye nyumba hizo,” alisema Lukuvi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Zakia Meghji, alisema watatekeleza maagizo yote waliyopewa.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema katika mradi wa Lugurudi, nyumba zitauzwa kuanzia sh. milioni 20.
Alimhakikishia waziri huyo kuwa, wataendelea kujenga nyumba za bei nafuu, ambazo zinalingana na maisha ya Mtanzania.
Katika ziara hiyo, Lukuvi alifuatana na Naibu Wake, Angelina Mabula, ambapo pia alilipongeza shirika hilo kwa mafanikio makubwa.
Alisema shirika lina hadhi kubwa na kwamba menejimenti inafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.


No comments:

Post a Comment