Wednesday 23 March 2016

TUMBUA TUMBUA WABUNGE YATIKISA, NDASSA, CHEGENI, LUGORA WATEMWA




HATIMAYE baadhi ya wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge na makamu wenyeviti wameenguliwa na wengine kuhamishwa kamati.
Wakati mabadiliko hayo yakifanyika kwa wenyeviti hao, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Zitto Kabwe, ameamua kuachia ngazi kupisha uchunguzi.
Sambamba za Zitto, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, naye alitangaza kuandika barua kwa Spika ili kujivua ujumbe wa kamati hiyo kwa sababu kama aliyoitoa Zitto.
Hatua ya kuenguliwa kwa wenyeviti na makamu wenyeviti hao imekuja huku kukiwa na tuhuma za kuwepo kwa vitendo vya rushwa miongoni mwao.
Taarifa ya Ofisi ya Bunge iliyotolewa jana, ilisema Spika wa Bunge, Job Ndugai, amefanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Ilisema mabadiliko hayo yamefanyika ili kuzingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda kamati hizo Januari, mwaka huu.
Taarifa ilisema baadhi ya kamati zitalazimika kufanya uchaguzi wa viongozi kutokana na waliokuwa wenyeviti au makamu wenyeviti kubadilishwa.
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii italazika kupata mwenyekiti na makamu mpya baada ya waliokuwepo kubadilishwa.
Kamati hiyo ilikuwa chini ya uenyekiti wa Mary Mwanjelwa. Chini ya mabadiliko mapya, Mary amehamishiwa Kamati ya Viwanda na Biashara .
Pia, Kamati ya Nishati na Madini inahitaji kupata mwenyekiti mpy, baada ya aliyekuwa akiiongoza Martha Mlata, kuhamishiwa Kamati ya Viwanda na Biashara.
Mabadiliko mengine yanamhusu Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Richard Ndassa, ambaye amehamishiwa Kamati ya Katiba.
Kangi Lugola, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Dk. Raphael Chegeni, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, wameondolewa.
Taarifa ya Ofisi ya Bunge ilitaja majina ya wabunge waliohamishwa kamati na kamati wanazokwenda kwenye mabano kama ifuatavyo:
Dk. Mary Mwanjelwa (Ardhi kwenda Viwanda), Martha Mlata (Nishati kwenda Viwanda), Richard Ndassa (PIC kwenda Katiba), Suleiman Zedi (PIC kwenda Katiba) na Victor Mwambalaswa (LAAC kwenda Mambo ya Nje).
Wengine ni  Dk. Raphael Chegeni (Huduma za Jamii kwenda Mambo ya Nje), Kangi Lugola (LAAC kwenda Mambo ya Nje) na Margaret Sitta (Huduma za Jamii kwenda Utawala).
Pia, wamo Abdulaziz Abood (Viwanda kwenda LAAC), Suleiman Nchambi (Viwanda kwenda Katiba) na Ibrahim Raza (Viwanda kwenda Utawala/Serikali za Mitaa).
Mabadiliko mengine yanawahusu Emmanuel Mwakasaka (kutoka LAAC kwenda miundombinu), Suleiman Ahmed Sadick (LAAC kwenda huduma za jamii) na Sixtus Mapunda (Ardhi kwenda Ukimwi).
Vilevile Hamoud Abuu Jumaa ametolewa Ardhi kwenda Utawala/Serikali za mitaa, Wilfred Lwakatare (Ardhi kwenda nishati) na Boniphace Getere (Ardhi kwenda huduma za jamii).   
Aidha, baadhi ya viongozi ambao wamefanyiwa mabadiko, wanadaiwa kujihusisha na suala la rushwa kinyume na sheria za nchi.
Tarifa ambazo zilitoka ndani ya Ofisi ya Bunge zilieleza kuwa, katika ripoti aliyokabidhiwa Spika Ndugai, ilikuwa inahusu mwenendo wa bunge.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika ofisi hizo, utendaji wa kamati hizo hauridhishi kutokana na baadhi ya viongozi na wabunge kujihusisha na rushwa.
Ilidaiwa kuwa baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikiombwa au kushinikizwa kutoa rushwa.
Baada ya  ripoti hiyo kufika kwa spika, jana alifanya mabadiliko hayo rasmi, ambapo alieleza lengo ni kukabiliana na changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa kamati hizo.

No comments:

Post a Comment