JESHI la polisi limesema linaendelea na uchunguzi iwapo
kuna ukweli wowote juu ya madai ya kutekwa kwa mwandishi wa gazeti la Mwananchi
na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW), Salma Said Humud.
Pia, limetangaza kuyaua majambazi matatu yaliyokuwa
yakikusudia kupora katika duka la kubadilishia fedha, Masaki, wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam.
Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Simon Sirro, akizungumza juzi, jijini Dar es Salaam, alisema si kila madai ni
kweli ama uongo, hivyo uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli.
“Alipatikana jana, tukapata taarifa yuko hospitali ya
Regency, tulituma wapelelezi, walimhoji, ambapo alidai alitekwa juzi na watu
asiowafahamu mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere na kupelekwa mahali asipopafahamu, ambapo aliachiwa jana
alfajiri akiwa salama,” alisema.
Alisema ni mapema kwa jeshi hilo kusema iwapo suala hilo
linaukweli wowote ama ni uongo, hadi upelelezi utakapokamilika.
“Hata hivyo, si hali ya kawaida mtu kutekwa halafu
kuachiwa bila madhara huku akiwa na vifaa vyake vyote, upelelezi unaendelea ili
kubaini ukweli,” alisema.
Alisisitiza kuwa baada ya kukamilika kwa upelelezi,
hatua zitachukuliwa dhidi ya waliohusika iwapo ni kweli, vilevile jeshi hilo
halitasita kuchukua hatua iwapo madai hayo si ya kweli.
Wakati huo huo, jeshi hilo limewaua majambazi watatu,
ikiwa ni pamoja na kukamata silaha tatu aina ya bastola, eneo la Masaki Mwisho,
Dar es Salaam, waliokuwa na dhamira ya kupora katika duka la kubadilishia
fedha.
Kamishna Sirro, alisema hatua hiyo ni kufuatia
operesheni maalumu inayoendeshwa sasa katika jiji la Dar es Salaam, ambapo
jeshi hilo lilipokea taarifa za kuwepo kwa njama hizo za ujambazi.
“Majambazi hao walikuwa na gari aina ya RAV 4, lenye
namba za usajili T125 BQJ, ambapo walipowaona askari, walianza kuwafyatulia
risasi na askari hao kujibu mashambulizi yaliyofanikisha kuyaua matatu,”
alisema.
Mbali na bunduki hizo, alivitaja vitu vingine
vilivyokutwa navyo ndani ya gari hilo kuwa ni hirizi mbili, nyekundu na nyeusi,
karatasi nyeupe yenye maandishi mekundu yaliyoandikwa kiarabu, simu tatu,
nyundo moja na bomu la kurusha kwa mkono.
Kamanda Sirro alisema katika eneo la Mbagala kwa Mponda,
jeshi hilo lilikamata silaha moja aina ya bastola, baada ya abiria wa bodaboda
aliyetaka kuporwa na majambazi, kurusha risasi kwa bastola yake anayomiliki
kihalali, ndipo majambazi hayo yalidondosha bastola yao wakati wakikimbia.
“Tunawataka wahalifu hususani wanaotumia silaha, kuacha
biashara hiyo kwani hailipi na kwa uzoefu wetu mwisho wa watu kama hao huwa ni
mbaya, watafute ajira zingine,” alisema Sirro.
Kamanda huyo alisema katika kipindi hiki cha kuelekea
sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limejipanga
vema kukabiliana na uhalifu na kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu.
“Jeshi litahakikisha Dar es Salaam inakuwa shwari,
tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kuripoti pindi wanapoona dalili za uvunjifu wa amani,” alisema.
Alisema jeshi hilo litafanyakazi hiyo kwa kushirikiana
na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Kikosi cha Polisi Wanamaji, ulinzi
shirikishi na kampuni binafsi za ulinzi ili kuhakikisha usalama kwa raia na
mali zao.
Alisema miongoni mwa maeneo watakayolinda ni nyumba za
ibada, ikiwemo misikiti na makanisa, fukwe za bahari, nyumba za starehe na
mitaani, ambapo ‘disko toto’ zimepigwa marufuku.
No comments:
Post a Comment