Wednesday, 23 March 2016

NITAKIIMARISHA CHAMA KIITIKADI-OLE SENDEKA


MSEMAJI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, amesema atahakikisha anatumia vema nafasi aliyopewa kwa kukiimarisha Chama kiitikadi.
Ole Sendeka, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Simanjiro, mkoani Manyara, alisema hayo jana, alipozungumza na Uhuru, Dar es Salaam.
Alisema amepokea kwa furaha kubwa uteuzi huo na kwamba, atahakikisha hakiangushi Chama na atakuwa mstari wa mbele kutetea sera na itikadi.
“Moja ya majukumu yangu ni kufafanua mafanikio ya utekelezaji wa Ilani  na changamoto zitokanazo na utekelezaji huo,” alisema Ole Sendeka.
Alisema kazi nyingine atakayoifanya kama msemaji wa Chama ni kukiimarisha kiitikadi, hivyo aliwaomba wanachama na wananchi kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Akizungumzia wapinzani, aliwaomba waelewe kuwa nchi ni moja, hivyo hawana budi kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Ole Sendeka aliteuliwa na Chama  kushika wadhifa huo, baada ya aliyekuwa msemaji, ambaye ni Katibu wa Taifa wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Akitangaza uteuzi huo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema nafasi hiyo kwa sasa inachukuliwa na Ole Sendeka baada ya Nape kupewa majukumu ya kiserikali.

No comments:

Post a Comment