Wednesday, 23 March 2016

CCK KUANDAA MAANDAMANO YA KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI NCHI NZIMA


ALIYEKUWA mgombea urais, kupitia Chama Cha Kijamii (CCK),
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Dk. Godfrey Malisa, anatarajia kuitisha maandamano ya nchi nzima yenye lengo la kumpongeza Rais Dk. John Magufuli na serikali.

Maandamano hayo yatakayofanyika mwishoni mwa Aprili
mwaka huu, yanatarajiwa kufanyika katika mikoa yote nchini na
kupokelewa na wakuu wa mikoa husika.

Akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Dk. Malisa, ambaye pia alikuwa miongoni mwa wagombea wa kiti cha uspika katika bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema maandamano hayo yamelenga kudumisha umoja wa Watanzania.

Dk. Malisa alisema maandamano hayo, ambayo yatahusisha wananchi wote na kutokuwa na itikadi, hayatatoa fursa kwa chama chochote cha siasa, kutoa hisia zao za kisiasa, badala yake yatakuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali na kupeana hamasa ya kuwasaidia viongozi kulijenga taifa.

Akizungumzia sababu zilizomsukuma kuandaa maandamano hayo, Dk. Malisa alisema ni baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli pamoja na serikali yake katika kudhibiti mianya ya rushwa, ufisadi na mafisadi katika miezi mitano ya awali ya utawala wake.

Aidha, alisema kutokana na juhudi zilizoonyeshwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. Magufuli, ni wazi kwamba wananchi wanapaswa kuunga mkono kazi hizo na kushiriki kumtia moyo rais, pamoja na kumwombea kutimiza ahadi alizozitoa kwa wananchi.

Kuhusu maandamano hayo, alisema hivi sasa anaendelea kuwasiliana na waratibu mbalimbali katika mikoa yote nchini, ili kuhakikisha azma hiyo inafikiwa kwa kuwa na washiriki kutoka katika kada mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dk. Malisa, mikoa kadhaa imeonyesha mwitikio na kukubali kushiriki katika maandamano hayo, ikiwemo mikoa ya Mbeya, Iringa, Manyara, Kilimanjaro, Arusha na Dar es Salaam.

Dk. Malisa ameyafananisha maandamano hayo ana yale ya wananchi waliounga mkono Azimio la Arusha, lililoasisiwa na Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere, yaliyofanyika bila kujali itikadi za dini, siasa na tofauti zingine zozote bali walitanguliza mbele maslahi ya taifa.

Maandamano hayo yasiyokuwa na itikadi za dini au vyama vya siasa, yatashirikisha makundi yote ya kijamii, wakiwamo wasomi, wafanyakazi, wafanyabiashara wa kada zote na wananchi wa kawaida, lengo likiwa kutaka Watanzania kuwa na mabadiliko.

No comments:

Post a Comment