Wednesday, 23 March 2016

DIWANI CCM MERU AFARIKI DUNIA



CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Meru kimepata pigo baada Diwani wake katika Kata ya Ngarenayuki, Naftal Mbise, kufariki dunia.

Marehemu Mbise alifariki ghafla jana, katika Hosptali ya Tengeru wilayani humo.

Mbise alikuwa diwani pekee wa CCM katika Halmashauri ya Meru, baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

Akithibitisha kufariki kwa diwani huyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Bakari Sajini, alisema kutwa nzima jana, marehemu alikuwa mzima, akiendelea na shughuli zake za kila siku.

Alisema ilipotimia saa tisa alasiri, alirejea nyumbani kwake kisha kuchukua ngazi kwa ajili ya kukata tawi la mti, ambalo lilikuwa  linakwaruza kwenye paa la nyumba, lakini kwa bahati mbaya aliteleza na kuanguka.

Alisema baada ya kuanguka, alikimbizwa kituo cha afya cha Ngarenanyuki na kubainika kwamba, amevunjika mguu na alikuwa na maumivu makalali mgongoni, ambapo alipatiwa huduma ya kwanza  na kupelekwa Hosptali ya Wilaya ya Tengeru.

"Wakati madaktari wa Hospitali ya Tengeru wakifanya jitihada za kuokoa maisha yake, alifariki dunia saa 3.30 usiku,” alisema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Langael  Akyoo, alisema amepokea taarifa za msiba huo kwa mshtuko mkubwa kwani  marehemu alikuwa kipenzi cha wananchi wote wa Meru kutokana na utendaji kazi wake mzuri kwa jamii.

Alisema mazishi yake yatafanyika  Machi  26, mwaka huu, nyumbani kwake, Mwakeni, kata ya  Ngarenayuki.

No comments:

Post a Comment