Thursday 24 March 2016

ZANZIBAR HAPATOSHI LEO


RAIS Mteule wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, anatarajiwa kuapishwa leo kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuongoza viongozi mbalimbali, wakiwemo wageni mashuhuri katika sherehe hizo.

Muda mfupi baada ya Dk. Shein kutangazwa mshindi, Rais Magufuli alimtumia salamu za pongezi, akimtakia kila la kheri pamoja na wananchi wa Zanzibar.

Mbali na Rais Dk. Magufuli, viongozi wa nchi mbalimbali wamekuwa wakitoa salamu za pongezi kwa Dk. Shein, wakimtakia afya njema na utendaji bora katika miaka mitano ya uongozi wake.

Dk. Shein, alipata ushindi wa kishindo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, Machi 21, mwaka huu, alimtangaza Dk. Shein kuwa Rais Mteule wa visiwa hivyo, ambavyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Jecha, alimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi baada ya kupata kura 299,982, sawa na asilimia 91.4, kati ya kura 341,865, zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo uliokuwa wa amani na utulivu, idadi ya wapigakura ilikuwa 503,580 na zilizoharibika ni 13,327. Vyama 14 vilishiriki.

Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, alisema jana kuwa, maandalizi yamekamilika na ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo.

Vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi vilikuwa vikiendelea na maandalizi kwenye Uwanja wa Amaan, kwa ajili ya kujiandaa na sherehe hizo.

Ratiba inaonyesha kuwa, sherehe za kuapishwa Dk. Shein, zitaaanza saa 1:30 asubuhi na wageni mbalimbali, wakiwemo viongozi wa ndani na nje, watahudhuria.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetangaza kuwa leo ni siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa watumishi wa umma na wananchi, kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Hali ni shwari katika visiwa vya Unguja na Pemba na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika maeneo yote ya mjini hapa.

Akizungumza na waandishi jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga 'Mawe Matatu', aliwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo.

Kitwanga alisema usalama wa raia na mali zao utakuwa mkubwa na hadi kufikia jana, hakukuwa na taarifa zozote kuhusu watu au kundi linalojiandaa kuleta vurugu.

Alisema hakuna mtu aliyekamatwa kwa kuhisiwa kutaka kuleta vurugu na kuongeza kuwa, vyombo vyaulinzi vinafanya doria usiku na mchana kuhakikisha Zanzibar inakuwa shwari.

"Kama mnavyoona kabla na baada ya uchaguzi, hali ya usalama ni nzuri, wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na tunaamini hali hii itakuwa ya kudumu," alisema Kitwanga.

Aidha, alisema watu 30 waliokamatwa kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba za makazi au ulipuaji wa mabomu, wanaendelea kuchunguzwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Wananchi, wanachama na mashabiki wa CCM, waliwasili kwa wingi jana kutoka Pemba, kujumuika na wenzao wa Unguja katika sherehe hizo, wakiwa wamevaa sare za CCM.

Mbali na Dk. Shein, wagombea wengine wa urais waliopigiwa kura katika uchaguzi huo ni Khamisi Idd Lila wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 1,225, Juma Ali Khatibwa  ADA-TADEA (1,562), Hamad Rashid Mohammed wa ADC (9734).

Wengine ni Said Soud Said wa AFP (1,303) Ali Khatib Ali wa CCK (1,980), Mohammed Masoud Rashid wa CHAUMMA (493) Seif Sharif Hamad wa CUF (6,076) na Tabu Mussa Juma wa D-MAKINI (210).

Wagombea wengine walikuwa Abdallah Kombo Khamis wa DP (512), Kassim Bakari Ali wa Jahazi Asilia (1,470) Seif Ali Idd wa NRA (266), Issa Mohammed Zonga wa SAU (2,018) na Hafidh Hassan Suleiman wa TLP, aliyepata kura 1,496.

Uchaguzi Mkuu wa marudio ulifanyika Machi 20, mwaka huu, baada ya ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali, uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kutokana na kubainika kuwepo kwa dosari nyingi.

Katika hatua nyingine, Dk.  Shein amezidi kupokea pongezi baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemesema ushindi huo unaashiria imani kubwa ya Wazanzibari kwa Dk. Shein na CCM kwa ujumla.

Mbali na CCM, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  (UVCCM), umesema ushindi huo ni kielelezo cha kuimarika kwa demokrasia ya Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, kwa vyombo vya habari, ilisema inawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo na kutimiza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaofaa.

“CCM inawatakia kila la kheri Rais Mteule Dk. Shein, wawakilishi na madiwani wote katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kwamba, tunaamini kupitia wao, kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” itatekelezwa kwa umakini mkubwa,” alisema.

Aidha, CCM imewahimiza wananchi wa Zanzibar kudumisha umoja na mshikamano katika kuijenga Zanzibar yenye mafanikio.

UVCCM imesema ushindi alioupata Dk. Shein ni kielelezo cha kuimarika kwa demokrasia ya Zanzibar.

Umesema ushindi huo sasa umehitimisha mvutano na maneno yaliyokuwa yakienezwa kwa makusudi na kupotoshwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani visiwani humu.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo katika Ofisi Kuu ya UVCCM Zanzibar, iliyoko Kikwajuni, wakati akizungumza na wandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa maandamano makubwa yaliyoandaliwa na umoja huo kusherehekea ushindi wa CCM.

Alisema ushindi alioupata Dk. shein wa asilimia 91.4, umeidhihirisha dunia jinsi ya kukubalika kwa kiongozi huyo na uongozi wake.

"Ameonyesha umahiri, upeo na uwezo mkubwa  katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa kwa miaka mitano iliyopita. Amekuwa mstahamilivu na nguzo muhimu ili jamii isiendelee kugawanyika,"alisema Shaka.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM, alisema aina ya uongozi wa Dk. Shein ni wa kipekee na kwamba, kama angekuwa si mtawala mwenye maarifa mapana na uvumilivu wa kisiasa, serikali hiyo ingevunjika mapema.

Shaka alisema serikali za mseto za Zimbabwe na Kenya ziliweza kuyumba na kwamba, hazikudumu kutokana na baadhi ya viongozi wake kukosa kuaminiana, kuvumiliana na kustahamiliana.

"Ushindi huu ni pigo jipya kwa CUF, ambacho kimesusia uchaguzi wa marudio bila sababu za msingi. Ushindi wa Dk. Shein naamini utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kuishangaza dunia katika maendeleo ya demokrasia," alisema Shaka.

Aliongeza kuwa anatarajia serikali mpya ijayo haitakuwa na viongozi wababaishaji, badala yake watateuliwa wazalendo, wachapakazi na watu wenye uchungu wa kuyatetea Mapinduzi bila kushiriki usaliti.

Shaka alisema anaamini kuwa chini ya uongozi wa kipindi cha pili cha utawala wa Dk. Shein na sera makini za CCM, ataendelea kusimamia uadilifu serikalini, kujenga umoja wa kitaifa nchini na kuwatumikia wananchi ipasavyo na kudumisha huduma za jamii.

"UVCCM tuna matumaini makubwa na Dk. Shein katika awamu mpya ya ushindi wake, ataunda baraza la mawaziri makini na hatutosita kumpongeza kila atakapofanya vizuri. Pia hatutakaa kimya pale tutakapoona mambo hayaendi ipasavyo,"alisema.

Shaka aliwahimiza vijana mahali popote walipo, kumuunga mkono Dk. Shein na kuisaidia serikali yake ili iweze kupiga hatua za kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment