Wednesday 12 October 2016

WAZIRI MWAKYEMBE AFICHUA SIRI NZITO

WAZIRI wa Katiba  na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, amefichua mikakati mizito, inayofanywa na baadhi ya mashirika na matajiri wakubwa duniani, kutaka kuigeuza Tanzania kuwa  kitovu kikuu  cha ushoga na usagaji  barani Afrika.

Amesema  tayari serikali imefanikiwa kunasa nyaraka muhimu  za ushahidi zinazodaiwa kutumika na baadhi ya asasi za ndani na nje ya nchi, kujaribu kueneza ushoga na kwamba, mkakati huo umelenga kuifanya mikoa 11, kuwa ngome ya ushoga hapa nchini.

Dk. Mwakyembe aliitaja mikoa hiyo  kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma,  Arusha, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Morogoro, Lindi, Kilimanjaro na Njombe, ambapo alisema tayari taasisi hizo zimeanza kujaribu kuhamasisha na kutoa mafunzo ya jinsi ya kushiriki vitendo hivyo.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa asasi  15,  za kitaifa na kimataifa, zinazojihusisha na ufanikishaji wa mpango huo na kwamba, unafahamika kama MSM, ikimaanisha 'Man having Sex with Man'.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana, Dk. Mwakyembe alisema asasi hizo zimemwaga fedha nyingi na  magari katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa.

Kufuatia hali hiyo,  Waziri Dk. Mwakyembe alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, Profesa Sifuni Mchome,  kukutana haraka na makatibu wakuu  wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara  Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili kujadili suala hilo.

Pia, aliagiza kufanyika kwa  tathimini ya kina juu ya nyaraka zilizonaswa  na serikali,  zinazodaiwa kutumiwa katika uhamasishaji huo maeneo mbalimbali ya nchi na kuchukua hatua stahiki kuliepusha taifa na janga hilo.

Alisema nyaraka hizo ni pamoja na vitini, majarida na machapisho mbalimbali,  ambavyo  asasi hizo zilikuwa zikijaribu kuvitumia kuhalalisha ushoga kwa  watoto  katika shule za msingi na sekondari nchini.

"Nawapa wiki mbili makatibu hao kutoa majibu juu ya nyaraka hizo na kuthibitisha kwa maandishi kuhusu  asasi hizi, zinazojifanya kuendesha mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) wakati zinalenga kuhamasisha ushoga,” alisema waziri huyo.

Aliongeza: “Makatibu hawa watueleze ni wapi tumejikwaa kiasi cha  kufikia hapa. Mimi na mawaziri wenzangu katika wizara husika tuletewe hatua za haraka tunazotakiwa kuchukua, ambazo zitakuwa za muda  mfupi na mrefu."

Waziri huyo alisema kikao hicho cha makatibu wakuu pia kitoe mapendekezo ya hatua za kuzichukuliwa asasi hizo, ambazo zimejiingiza katika uhamashaji wa ushoga nchini.

"Tunatakiwa kujua madhara, ambayo tayari tumepata, hasa kwa watoto na vijana, ambao wameshawishiwa na kuathirika na vitendo hivyo mpaka sasa,” alisema Dk. Mwakyembe.

Aliongeza: “Naagiza kuanzia sasa yeyote tutakaye mkamata anajihusisha na uhamasishaji wa ushoga na mapenzi ya jinsia moja,  bila kusubiri uchunguzi unaofanywa na makatibu wetu, tutamshughulikia.”

Aidha, aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kuanza kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya ushoga na mapenzi ya jinsia moja.

"Daima serikali haiwezi kuthubutu  kuridhia sheria yoyote inayohusu ushoga au ndoa za jinsia moja kwa sababu ni kinyume cha katiba, sheria na kanuni za nchi. Tuko tayari  kuona taifa likikosa misaada  kutokana na kupinga ushoga na ndoa za jinsia moja na hatutakubali taifa letu kugeuzwa kuwa kitovu cha ushoga,” alisema Dk. Mwakyembe.

Aliongeza kuwa serikali inajua kila kitu kinachoendelea kuhusu ushoga, hivyo aliwatoa hofu wananchi kwamba, ipo imara katika kupambana nalo kwa nguvu zote.

“Kinachouma zaidi ni kwamba, watu hawa wanalenga watoto wadogo  walioko katika shule za msingi na sekondari. Pia, wanatumia mikutano ya siri usiku kuchapisha na kuandaa vipeperushi, majarida na kuandaa sherehe za chakula,”alibainisha.

Aidha, alisema wamekuwa wakisambaza vilainishi vinavyotumika wakati wa kushiriki mapenzi ya jinsia moja na kondom.

Dk. Mwakyembe alisema baada ya uchunguzi huo, atayaanika hadharani mashirika, asasi na matajiri walio nyuma ya mkakati huo.

SHINIKIZO LA KURIDHIA USHOGA

Waziri Dk. Mwakyembe alisema shinikizo la mataifa makubwa duniani juu ya Tanzania kuridhia ndoa za jinsia moja na ushoga, liliibuka katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu, uliofanyika Geneva, Uswisi mwezi uliopita.

“Walituhumu kuwa Tanzania  kuna ukiukwaji mkubwa wa kaki za binadamu  na kwamba, tunaruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja. Pia walihoji  kuhusu sheria yetu ya ndoa ya mwaka 1971, kwamba ni kandamizi kwa mtoto wa kike na kwamba, tumekuwa tunakiuka  kuwapa huduma za matibabu  waathirika wa ukimwi,” alibainisha.

Aliogeza: "Madai hayo yote si ya kweli, hatujawahi kuwa na sheria au sera ya kubagua mtu ama kundi katika kumpa matibabu mwathirika wa ukimwi.”

No comments:

Post a Comment