Monday, 1 May 2017
WAFANYAKAZI WALIPWE MALIPO WANAYOSTAHILI-TUCTA
SHIRIKISHO la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limewataka wafanyakazi nchini kutimiza wajibu wao kwa kufanyakazi kwa bidii na nidhamu ili waweze kulipwa malipo yanayostahili.
Aidha, TUCTA imesema ili serikali iweze kufanikisha mpango wake wa kujenga Tanzania ya viwanda, inapaswa kuwa na ushirikiano wa karibu na waajiri na waajiriwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Yahaya Msigwa, alipokuwa akizungumza na Uhuru, mwishoni mwa wiki iliyopita, kuhusu maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi, ambayo kitaifa yanafanyika leo mkoani Kilimanjaro.
Msigwa alisema iwapo wafanyakazi hawatakuwa na nidhamu na wataendeleza vitendo vya wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, haitakuwa rahisi kwa mpango huo wa ujenzi wa Tanzania ya viwanda kufanikiwa.
Alisema wafanyakazi wanapaswa kutimiza wajibu wao ili walipwe haki wanazostahili, lakini pia serikali inapaswa kuwa karibu na wafanyakazi na waajiri ili kuwe na amani katika maeneo ya kazi na uzalishaji uwe bora.
Kwa mujibu wa Msigwa, makundi hayo matatu hayapaswi kudharauliana kwa upande mmoja kujiona bora kuliko mwingine, vinginevyo uzalishaji hautakuwa na tija.
"Kila kundi linamhitaji mwenzake, ukilidharau kundi jingine, unajidanganya,"alisisitiza.
Aliongeza kuwa siku zote mfanyakazi anapaswa kuheshimiwa na mwajiri wake, vivyo hivyo mwajiri naye anapaswa kumuheshimu mfanyakazi wake kama ambavyo serikali nayo inapaswa kuyaheshimu makundi hayo mawili.
"Hakuna mfanyabiashara anayetaka kupata hasara, vivyo hivyo hakuna mfanyakazi anayetaka kutumia nguvu zake bila kulipwa haki anazostahili. Makundi haya yanategemeana, hivyo yakiungana pamoja, lazima tija ipatikane sehemu yoyote ya kazi,"alisema.
Msigwa alisema mambo muhimu katika utendaji wa kazi ni rasilimaliwatu, fedha, mitambo na muda na kwamba, iwapo vitu hivyo vitatumika vizuri, kutakuwepo na ufanisi mzuri katika utendaji wa kazi.
Katibu Mkuu huyo wa TUCTA alisema katika miaka ya 1970, uchumi wa Tanzania ulikuwa sawa na wa nchi za Korea, Singapore na Indonesia, lakini uchumi wa nchi hizo kwa sasa upo juu zaidi kutokana na kutumia vyema rasilimali ilizonazo, hasa watu.
Msigwa alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi, yakiwemo madini, mbuga za wanyama na makaa ya mawe, ambazo zikitumika vizuri, uchumi wa nchi utapaa na kuwa wakati na ajira zitaongezeka.
Mtendaji huyo mkuu wa TUCTA alisema, kosa kubwa lililofanywa na serikali ni kuanza mapema uchimbaji wa madini kabla Watanzania hawajawa na elimu ya kutosha kuhusu rasilimali hiyo.
"Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alitutahadharisha kuhusu hilo kwa kututaka tusubiri kuelimika kwanza ndipo tuanze kuchimba madini. Pia, alitutahadharisha tusiwakaribishe wazungu kuja kuchimba madini kwa kuwa watatuibia na hicho ndicho kilichotokea,"alisema.
Akitoa mfano, Msigwa alisema madini yaliyoko Ghana, ambayo ni miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati ni 1/10 ya madini yote yaliyoko Tanzania, lakini yamekuwa yakichangia asilimia kati ya 40 hadi 50 katika uchumi wa nchi hiyo.
Alitoa wito kwa wafanyakazi nchini kuwa na nidhamu na kuongeza bidii katika kazi huku waajiri nao wakiwalipa vizuri wafanyakazi wao kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment