Monday, 1 May 2017

JPM AUAGIZA UONGOZI MKOA WA KILIMANJARO KUTATUA KERO ZA WANANCHI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Aprili 2017, amekutana na kuzungumza na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali na kuuagiza uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kutatua kero zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko ya baadhi ya viongozi wa dini kueleza kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na manyanyaso yanayofanyiwa na wafanyakazi wa Wakala wa Maegesho ya magari mkoani humo.

Kufuatia malalamiko hayo, Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU kuchunguza mkataba uliongiwa kati ya Manispaa ya Moshi na Wakala wa Maegesho ya magari mkoni humo ili kujua uhalali wake kwani kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa upotevu wa mapato yatokanayo na makusanyo ya maegesho hayo.

‘Uangalie ule mkataba wa parking wa hapa Moshi,kama kuna ufisadi wowote peleka Mahakamani,lakini haya ya administration kayaangalie wasinyanyase watu, huwezi hata ukamuona sheikh unafunga gari lake,ukimuona Mchungaji na kola yake unafunga tu ni ushetani, sasa saa nyingine wale vijana wanaofanya ile kazi wanajisahau, hawaheshimu utu wa Watanzania’–Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Manisapaa ya Moshi kutoa kibali cha Ujenzi wa Kituo cha Uchunguzi wa maradhi kilichoombwa na mwananchi mmoja mkoani humo ili aweze kuendelea na ujenzi huo kutokana na kutopewa kibali hicho kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kutokana na Serikali kuzuia unywaji wa pombe aina ya viroba idadi ya vifo katika mkoa wa Pwani imepungua kutoka 80 hadi 20 na hata ajali za pikipiki maarufu Bodaboda nazo zimepungua nchini.

Aidha, Rais Magufuli ametaka uongozi wa Wilaya ya Hai kufanya kazi bila kutishwa na madiwani ikiwa ni pamoja na kubadili sheria ndogondogo wilayani humo ili kupunguza kero za utitiri wa ushuru kwa wananchi.


Rais Magufuli ametoa maagizo hayo wakati alipokutana na viongozi wa dini wa mkoa wa Kilimanjaro, Vyama vya Siasa na watendaji wa Serikali mkoani humo na kula nao chakula cha mchana kilichoandaliwa na mkoa wa Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment