Sunday, 30 April 2017

WATANZANIA TUONE FAHARI KUJIVUNIA MUUNGANO WETU- DK SALIM AHMED SALIM



Na Judith Mhina – MAELEZO

Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Kwanza Dkt Salim Ahmed Salim  amesema ili muungano wa Tanganyika na Zanzibar uweze kudumu na kuimarika hatuna budi kuelezea mafanikio yalitopatikana na pia kutafuta ufumbuzi wa kero chache zilizopo.

Dkt, Salim Ahmed Salim amesema hayo leo jijini Dar Es salaam wakati wa mahojiano na Idara ya Habari – MAELEZO kuhusiana namaadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika hizi karibuni.

Warizi huyo msataafu amekiri kwamba Watanzania wana haki ya kujivunia muungano huu ambao ni wa asili kutokana na mahusiano yetu ya kindugu hata kabla ya Muungano.  “Mahusiano ya kindugu baina ya Wananchi wa Tanganyika na Zanzibar ni ya miaka mingi ambapo watu wake wamekuwa wakitembeleana na kuoana. Aidha, mahusiano hayo yameonekana katika masualoa ya kijamii kama vile lugha, dini n.k.

Dkt Salim ameeleza kwamba, walichokifanya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekh Abeid Amani Karume ni kuweka uwazi juu ya mahusiano ya watu wa Tanganyika na Zanzibar duniani hususan kwa wale ambao hawajui asili ya watu wa pande hizo mbili.

 “ Jambo hili la Muungano kudumu miaka 53 linashangaza watu wengi duniani, hasa kwa dhana kwamba nchi za kiafrika zina matatizo, na sio rahisi kuelewana. Jambo  kubwa linalofanikisha  kudumu kwa Muungano wetu ni umoja, upendo na mshikamano. Tumekuwa tukuweka wazi mafanikio na pale penye changamoto hukaa pamoja na kuzungumza ili kuyapatia ufumbuzi.”

Akizungumzia suala la vijana kushika madaraka Serikalini, Dkt Salim amesema “Hii si jambo geni kwani  mimi ndiye kijana wa kwanza ambaye niliaminika nikiwa mdogo sana miaka 22 na kuteuliwa kuwa Balozi nchini Misri. Kazi hii haikuwa ndogo lakini niliifanya kazi kwa kujiamini na kwa uadilifu mkubwa huku nikipata maelekezo kutoka kwa viongozi wangu wakuu (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar).

Hivyo napenda kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa Watanzania wenzangu hususan vijana wanaoaminiwa na Taifa katika umri mdogo kushika uongozi wakubali nafasi hizo kwa kuwa bado wana nguvu ya kuweza kulitumikia Taifa letu. Lakini wasisahau kuwasikiliza viongozi waliowapa nafasi hizo, na ushauri wa wazee ni muhimu sana. Aidha, wajue kuwa nafasi za uongozi wanazomepewa kuwawakilisha Watanzania zilete maendeleo ya kweli.

Akielezea mustakabali wa maendeleo ya nchi, Dkt Salim alitolea mfano wa vijana wa Afrika ya Kusini ambapo hivi katibu alikwenda kushiki moja ya mikutano viongozi wa nchi za Afrika. hivi Amesema, vijana wa Afrika ya Kusini hawataki kusikia lolote zaidi ya mambo yanayowahusu wao na maisha yao. Hawajui kama kuna watu wamepigania uhuru na hatimaye ukombozi  wa nchi yao. Wao hilo si kipaumbele kwao, wanachotaka ni maendeleo ambayo yatagusa maisha yao.

“Hivyo ni vema Serikali zetu zilivyoamua kuelekeza nguvu katika viwanda vidogo vya kati na vikubwa, kwa sababu malighafi tunazo za kutosha ila tulikosa mbinu za kuongeza thamani ya malighafi zetu. “Nataka nikuhakikishie tuko kwenye njia sahihi ili kuwafanya vijana walio wengi washiriki katika kulijenga Taifa na kupata ajira ambazo zitawafanya waishi kwa furaha na matumaini,” Asema Dkt Salim.

Akijibu swali, kuhusiana na lipi la kujivunia kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Dkt Salim amesema : “ Umoja wetu ndio uliotufikisha miaka 53, tusingekuwa wamoja tungegawanyika na Muungano ungekuwa mashakani.  Angalia idadi kubwa ya Watanzania sasa ni wale waliozaliwa baada ya Muungano ambao hawajui lolote kuhusu Muungano.

Tuna Jukumu kubwa la kuendeleza elimu ya historia kwa vizazi vya sasa na vijavyo waelewe na kudhamini kazi zilizofanywa na waasisi wetu wa Muungano Mwalimu Nyerere na Shekh Karume. Mfano mzuri ni Taifa la China ambalo vijana wengi hawakuwahi kumuona Mao SeThung, lakini wanamjua kutokana na historia wanayoelezwa na matunda  yake ambayo wanayaona.

Pili, Watanzania tusibaguane kama alivyosema Mwalimu Nyerere kwamba dhambi ya ubaguzi haiwezi kuishia hapo unapombagua mtu, itaendelea kwa mwingine na mwingine na mwisho Taifa litagawanyika.

Aidha, Dkt Salim amesema kwamba Taasisi ya Mwalimu Nyerere itaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa muungano ambao ni tunda la umoja na mshikamano barani Afrika, hususani Tanzania ambao wanahitaji kuwa na elimu ya uraia.

Mwisho alimalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania kuuenzi na kudumisha muungano wetu ulioanzishwa na Waasisi wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekh Abeid Amani Karume.

No comments:

Post a Comment