MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, ametinga Mahakama ya Rufani Tanzania, kuongoza timu ya mawakili wa serikali, kuwasilisha hoja za kisheria katika rufani aliyoikata dhidi ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake.
DPP Mganga alikata rufani mahakamani hapo dhidi ya Kitilya na wenzake, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, wa kuitupilia mbali rufani yake, aliyoikata mahakamani hapo, akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwaondolea wajibu rufani hao shitaka la kutakatisha fedha.
Jana, Mkurugenzi huyo wa mashitaka akiongoza timu ya mawakili watano, akiwemo msaidizi wake, Oswald Tibabyekomya, waliiomba Mahakama ya Rufani kukubaliana na sababu zao za kukata rufani na kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu na kuielekeza isikilize rufani yao.
Ombi hilo waliliwasilisha mbele ya Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, Kipenka Musa na Augustine Mwarija, wakati rufani waliyoikata dhidi ya Kitilya na aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na mwanasheria wa benki ya Stanbic Tanzania, Sioi Solomon, ilipoletwa kwa kusikilizwa.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo, DPP Mganga alitambulisha timu yake anayoiongoza, akishirikiana na msaidizi wake, Tibabyekomya, Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis na mawakili wa serikali waandamizi, Shadrack Kimaro na Awamu Mbangwa.
Baada ya kuwatambulisha, DPP Mganga aliieleza mahakama kwamba, hoja zao za kukata rufani zitawasilishwa na msaidizi wake, Tibabyekomya, ambaye alidai wana sababu tatu za kukata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, uliotolewa na Jaji Mfawidhi, Moses Mzuna.
Tibabyekomya alidai malalamiko yao ni kwamba, jaji huyo wa Mahakama Kuu alikosea kwa kutoa uamuzi wa kufutwa kwa shitaka la nane la kutakatisha fedha, kwamba ulikuwa uamuzi mdogo.
“Kosa hilo lilikuwa linajitegemea lenyewe kama ilivyokuwa katika hati ya mashitaka, hivyo kuliondoa hakuna kilichobaki,” alidai na kuongeza kufutwa kwa shitaka hilo kulihitimisha shitaka kama lilivyoshitakiwa na uamuzi huo haukuwa mdogo ndani ya shauri na ulikuwa na madhara, kwani upande wa Jamhuri ulinyimwa haki ya kushitaki shitaka hilo.
Tibabyekomya alidai uamuzi ulitolewa na Mahakama Kuu, kwamba kuondolewa kwa shitaka hilo kulikuwa ni uamuzi ndani ya shauri, haukuwa sahihi kwa sababu hawakupewa haki tena ya kushitaki kosa hilo lililoondolewa.
“Tunasema hayo kwa sababu ukiangalia katika kumbukumbu, mahakama ya chini ilikataa baada ya kuwa imefuta shitaka hilo na kwamba haikuwa na uwezo wa kuruhusu kufanya mabadiliko au marekebisho ya hati ya mashitaka,” alidai.
Tibabyekomya alidai hoja zao ya pili na ya tatu katika rufani hiyo ni kwamba, jaji alikosea kusema kwamba upande wa jamhuri ulikuwa na haki ya kurekebisha shitaka, lakini haukutumika kabla ya kukata rufani.
Akielezea hoja hizo, Tibabyekomya alidai malalamiko yao ni kwamba, uamuzi wa Mahakama Kuu, jaji hakuangalia uamuzi wa mahakama ya chini kuhusiana na suala hilo, bali alichoangalia ni hoja zilizowasilishwa wakili wa wajibu rufani, Majura Magafu.
Alidai uamuzi kwamba upande wao ulikuwa na nafasi ya kufanya marekebisho au mabadiliko, ulifanyika wakati uamuzi wa mahakama ya chini, ambao uliwafungia milango ya kufanya hivyo, ulikuwa bado haujatenguliwa.
Tibabyekomya alidai uamuzi huo wa Mahakama Kuu usingeweza kutekelezeka kwa sababu uamuzi wa mahakama ya chini ulikuwa bado haujatenguliwa.
“Tunaomba sababu zetu za rufani zikubaliwe na Mahakama ya Rufani itengue uamuzi wa Mahakama Kuu na kuelekeza rufani ya upande wa jamhuri isikilizwe,” aliomba.
Kwa upande wa mawakili wa wajibu rufani, Dk. Ringo Tenga, Majura Magafu na Alex Mgongolwa, uliiomba mahakama hiyo kuitupilia mbali rufani hiyo kwa madai haina sababu za msingi za kisheria na imeletwa kabla ya wakati.
Wakili Magafu alidai rufani iliyokuwa imewasilishwa Mahakama Kuu iliwasilishwa kabla ya wakati kwa sababu uamuzi wa Mahakama ya Kisutu haukuwa na madhara kwani ulikuwa ni uamuzi mdogo.
Alidai uamuzi wa mahakama ya chini ulikuwa unatoa mwanya kwa upande wa jamhuri kama bado walikuwa wanataka kuendelea na shitaka hilo na kwamba, wanaruhusiwa kufanya hivyo wakati wa usikilizwaji.
Jopo la majaji lilimhoji Magafu iwapo hatua hiyo ingewasaidia upande wa jamhuri, ambapo alidai wanayo nafasi au mwanya wa kuomba kufanya marekebisho au mabadiliko katika mahakama ya chini.
Dk. Tenga alidai katika mahakama ya chini upande wa jamhuri haukuwasilisha maombi ya kufanya marekebisho au mabadiliko ya hati ya mashitaka na jaji wa mahakama kuu alisema wanayo nafasi ya kufanya hivyo.
Wakili Mgongolwa alidai upande wa jamhuri walikuwa na nafasi ya kufanya marekebisho au mabadiliko na kwamba, alichofanya jaji ni kuangalia iwapo uamuzi ule ulikuwa mdogo au la na hakusikiliza wahusika wa pande zote ili aamue kutengua uamuzi wa Kisutu au la.
Mgongolwa alidai iwapo jaji angetengua uamuzi huo, ndipo angekosea, hivyo rai yao ni kwamba rufani itupiliwe mbali kwa kuwa imeletwa kabla ya wakati.
Akijibu hoja za mawakili hao, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Mganga alisisitiza Mahakama ya Rufani inatakiwa itoe maelekezo kwa sababu Mahakama ya Kisutu imeshasema haina uwezo wakati Mahakama Kuu ikisema warudi wakafanye marekebisho.
Jopo la Majaji, lilitaka kujua kutoka kwa DPP kwamba, iwapo ikirudi Mahakama Kuu, rufani isikilizwe na jaji yule wa awali au la, ambapo DPP Mganga alijibu kwamba rufani hiyo itategemea maelekezo ya mahakama hiyo kwamba iende kwa jaji huyo au mwingine.
Baada ya kusikiliza kwa rufani hiyo, jopo hilo lilisema wahusika watataarifiwa tarehe ya hukumu.
No comments:
Post a Comment