Sunday, 30 August 2015

DK. SHEIN: UPINZANI WATAISOMA NAMBA



NA SULEIMAN JONGO

MWANZONI mwa wiki hii mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohammed Shein alichukua fomu kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikiwa ni sehemu ya hatua za kuelekea kuomba idhini ya Wazanzibari kuwania nafasi hiyo.

Baada ya uchukuaji fomu hizo, Dk. Shein ambaye kwa sasa ndiye Rais wa Zanzibar, aliwahutubia maelfu ya wazanzibari waliofurika katika Uwanja wa Demokrasia (Kibandamaiti) ambako alipata fursa japo kuwafahamisha wananchi kwamba amepanga kuwania tena urais.

Akiwaeleza wananchi kuhusu adhma yake hiyo alisema CCM imejipanga kushinda uchaguzi na hakuna wasiwasi kwamba si urais tu bali nafasi zote zinazowania kwenye uchaguzi huo ikiwemo uwakilishi, ubunge na udiwani zitachukuliwa na CCM kwa kuwa ndio Chama bora zaidi na kilicho na wagombea wenye uwezo wa kiuongozi.

Kwa mujibu wa Dk. Shein, upinzani utaendelea kuisoma namba katika uchaguzi mkuu huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema ushindi kwa CCM ni jambo lisilozuilika na kwamba Watanzania na Wazanzibari wajipange kupiga kura kwa uhuru na amani.

Dk. Shein alisema kwa namna CCM ilivyotekeleza ahadi zake ilizozitoa kupitia Ilani yake ya uchaguzi ya 2010, ni wazi kwamba Watanzania na Wazanzibari kwa namna ya pekee wataendelea kuiamini.

Alisema hakuna sababu kwa CCM kushindwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa imetekeleza ahadi zake na bado kupitia Ilani ya uchaguzi ya mwaka huuitaendelea kuahidi mambo ambayo inauhakika itayatekeleza.

"Ninachowahakikishia Wazanziri mwaka huu ni kwamba wapinzani wataisoma namba. Tutaendelea kushinda kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi uliopita," alisema.

Alisema anauhakika wa ushindi kwa CCM utakaotokana na misingi ya ukweli haki na amani si kwa hila kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Kwa mujibu wa Dk. Shein, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali yake imejitahidi kutekeleza mambo mbalimbali iliyoyaahidi kwa wapigakura.

AMSHANGAA MAALIM SEIF

Alisema shutuma za upinzani hususan makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba kuna matatizo kwenye tume ya uchaguzi, huo ni woga wa kisiasa unaotokana na kutokuwa na uhakika wa kushinda.

"Nawaomba wana-CCM endeleeni kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu. Kila mwenye haki ya kupiga kura atapata fursa ya kufanya hivyo bila bughudha.

"Sisi tutashinda tu kwa kuwa si mara ya kwanza. Tutashinda kihalali kwa kupigiwa kura na wananchi. Wanaolalamika kuibiwa kura wanazungumza mitaani bila kuonyesha ushahidi wa kisayansi.

Mbali na hilo alisema hakuna sababu ya kutishana kama wanavyofanya baadhi ya wagombea wa upinzani kwa kuwa CCM ni Chama cha waungwana wanaoheshimu taratibu.

"Sijaridhika na kauli za uongo zinazotolewa kwamba CCM tunaiba kura tutaenelea kulifanyia kazi. Kwenye vituo vya kupigia kura kuna wawakilishi wa vyama vyote sijui huo wizi wa kura unafanyika vipi.

"Kauli hizi si za kidemokrasia hususan kutoka kwa kiongozi aliyebobea, ni kauli zinazolenga kuleta vurugu na kuchochea uvunjifu wa amani," alisema.

Alisema mwenye dhamana ya kulinda kura iko kwenye vyombo husika si mwanasiasa wala chama chochote cha kisiasa.

IKIZIDI KUCHOKOZWA CCM ITAJIBU

Dk. Shein alisema kwa muda mrefu wana-CCM wamekaa kimya huku wanasiasa wengine wakiongea mambo mbalimbali ikiwemo kutoa vitisho.

"Kwa muda wote huo tumekaa kimya kwa kuwa hatuaoni sababu ya kujibizana wala kutishiana," alisema.

Alisema Tanzania ni kisiwa cha amani kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa uhuru.

Rais Shein alisema kutokana na ukweli huo ndiomana CCM haioni sababu ya kutoa vitisho kwa kuwa nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria.

Hata hivyo, alisema endapo wana-CCM wataendelea kuchokozwa watalazimika kujibu kwa kuwa si kwamba hawana cha kusema ila hawaoni haja ya kubishana vitu vilivyo wazi.

AKERWA VIONGOZI WA SOKA KWENDA MAHAKAMANI

Awali akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu hiyo, Dk. Shein alisema kuzorota kwa mpira wa miguu Zanzibar kunachangiwa na viongozi wa Cham cha Soka Zanziba (ZFA) kukimbilia mahakamani kwenye masuala ya kimichezo.

Alisema licha ya nia njema ya serikali yake kutaka kuimarisha michezo.

Dk. Shein aliyekuwa akijibu swali la mwandishi wa habari Farouk Karim aliyetaka kujua ni kwa jinsi gani amejipanga kuendeleza michezo kwenye serikali yake iwapo atachaguliwa tena, alisema sekta hiyo imeharibiwa na viongozi.

"Tatizo lipo kwa viongozi wa vyama vya mpira wanaokimbilia mahakamani. Serikali haiwezio kuingilia kati kwani mbali na mahakama sheria za Shirikisho la Mpira wa Miduu Duniani (FIFA) zinakataza serikali kuingilia mchezo huo.

"Naungana na wadau wa mpira kutaka katiba mpya ya mpira lakini inaonekana viongozi wenyewe hawapo tayari.

"Kwa namana hii kama hatutabadilika tutaendelea kuwa nyuma kwa muda mrefu," alisema.

Alisema serikali yake ipo makini kutekeleza iliyoyaahidi ikiwa ni pamoja na kuweka nyasi bandia katika uwanja wa  Amani na kujenga studio ya kisasa ya kuektia filamu.

Kwa mujibu wa Dk. Shein, amekuwa akifuatilia kwa karibu sekta ya michezo hususan mpira wa miguu lakini viongozi wa vyama vya micghezo hususan ZFA wamekuwa wazito kuitikia kasi yake kwenye maendeleo ya michezo.

"Wako baadhi ya vijana waliowahi kwenda nje kushiriki michuano mbalimbali na kufanya vizuri ambao nilihamasika kwa ushiriki wao niliomba niletewe niwapongeze na zawadi kawaandalia lakini hadi leo sijawaona.

"Hilo ndilo tatizo la viongozi wetu. Nakerwa na kusuasua kwa mpira wa miguu lakini sina jinsi kwa kuwa mambo haya hivi sasa yako mahakamani," alisema.

Kwa mujibu wa Rais Shein yuko tayari kuendelea kuipa nguvu sekta hiyo hususan pale viongozi wa michezo watakapokuwa tayari kushirikiana nae kwenye safari ya kuendeleza michezo.

ATABIRIWA KUIBUKA MSHINDI

Wengi wamkubali, unapofika Zanzibar hivi sasa habari ya mjini ni safu ya wagombea waliopitishwa na CCM kuwania nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza na Uhuru katika eneo la Maruhubi, Khamis Hamza Makame, alisema wingi wa wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatoa fursa kubwa kwa Dk. Shein kuibuka mshindi.

Makame alisema ni tofauti na uchaguzi uliopita, safari hii CCM itatangaza ushindi mapema kwa kuwa ndicho Chama chenye wafuasi wengi visiwani humo huku wale watakaopigia upinzani watagana na wagombea waliosalia.

"Tumeshazizoea siasa za Zanzibar lakini katika uchaguzi huu ni wazi kwamba Dk. Shein ataingia Ikulu mapema," alisema.

No comments:

Post a Comment