Monday 21 September 2015

SUMAYE: HEKA 300 NI KISHAMBA KIDOGO





WAKATI wakulima na wafugaji wilayani Mvomero, Morogoro wakiuana kutokana na tatizo la ardhi, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amesema shamba lenye ukubwa wa heka 300 analomiliki si lolote na kuwa ni dogo.
Amesema haoni tatizo kumiliki shamba hilo na kwamba, yapo mashamba ambayo watu wanazunguka kuyakagua kwa kutumia magari hivyo, haoni sababu ya watu kupiga kelele.
Pia amesema kuwa anamiliki shamba hilo kihalali na kuonyesha kushangazwa na baadhi ya wananchi wanaodai kuwa anamiliki eneo kubwa la ardhi.
“…Shamba la ekari 300 nalo unaweza kusema ni shamba… Hivi hujawahi kuona mashamba makubwa watu wanazunguka na magari,” alihoji Sumaye.
Kauli ya Sumaye imekuja wakati wananchi wa Mvomero wakilalamika na kuitaka serikali kumlazimisha kiongozi huyo arejeshe shamba hilo ikiwa ni sehemu ya kupunguza migogoro ya ardhi.
Kwa muda mrefu kumewepo na mapigano ya mara kwa mara baina ya wakulima na wafugaji wilayani humo kutokana na uhaba wa maeneo ya malisho ya mifugo na shughuli za kilimo huku baadhi ya vigogo wakidaiwa kumiliki maeneo makubwa bila kuyaendeleza.
Hata hivyo, tayari mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ameweka bayana kuwa mashamba yote ambayo hayajaendelezwa taratibu zitafuatwa ili kuhakikisha yanarudishwa chini ya serikali za vijiji kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
Amesema malalamiko ya wananchi wa Mvomero kuhusiana na wakubwa wachache kumiliki mashamba makubwa ambayo kwa sasa yamegeuka mapori, yamekuwa ya muda mrefu ni lazima hatua zichukuliwe.
Akizungumza jana katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha Azam TV, Sumaye alikiri kumiliki shamba hilo na kusisitiza kuwa si tatizo na analimiliki kihalali na alinunua kwa Chama cha Ushirika.
Hata hivyo, katika mahojiano hayo Sumaye alionekana kujiumauma na kushindwa kujibu kwa ufasaha baadhi ya maswali aliyokuwa akiulizwa ikiwemo kuzungumzia ufisadi.
Alisema kuwa ataendelea kupambana na suala la ufisadi kwa nguvu zote, lakini alipotakiwa kutaja majina ya watuhumiwa wa ufisadi waliowahi kutajwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, Sumaye alisema hawezi kuwataja.
Alidai kuwa hawezi kumtaja mtu fulani kuwa ni fisadi bila ya kueleza kinachomkabili hivyo, ataendelea kuukemea kila anapopata nafasi.
Kuhusu kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ambayo ilisababisha mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kujiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu, Sumaye alisema hajui mhusika wa kashfa hiyo.
Hata hivyo, alisema kuwa mara atakapomfahamu mhusika mkuu wa kashfa hiyo atamtaja, lakini kwa sasa hana anachofahamu.
Kwa nyakati tofauti akiwa ndani ya CCM, Sumaye alikuwa akimrushia makombora mazito Lowassa huku akimshutumu kuhusika kwenye kashfa mbalimbali na kuonya kuwa hastahili kuwa kiongozi wa taifa.
Sumaye, ambaye kwa sasa amejiunga na kundi la UKAWA licha ya kutofahamu atakuwa mwanachama wa chama gani kati ya vinavyounda genge hilo, alikwenda mbali na kuionya CCM kutompa nafasi Lowassa kuwania urais.
Aliwahi kukaririwa akionya kuwa atakuwa wa kwanza kukihama CCM iwapo kitampitisha Lowassa kuwa mgombea urais wake, ushauri ambao ulionekana kuungwa mkono na wanachama na viongozi wa CCM, ambapo alikatwa hatua za mwanzo za mchakato.
Hata hivyo, katika mkakati ambao bado haujafahamika vyema, Sumaye amekuwa mpigadebe mkuu wa Lowassa kwenye mikutano ya kampeni.

No comments:

Post a Comment