Monday 21 September 2015

KINANA, SHIRIMA WAMTIKISA MBATIA





KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka wakazi wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, kutofanya makosa ya kuchagua mbunge na madiwani kutoka upinzani.
Amesema wagombea wa vyama hivyo hawana sera wala dhamira njema ya kuwatumikia watanzania na badala yake wachague wagombea wa CCM kuanzia rais, wabunge na madiwani.
Aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Innocent Shirima, mgombea urais Dk. John Magufuli na madiwani wa chama hicho.
Alisema CCM ndio chama pekee kinachoweza kuwaletea maendeleo ya haraka, kutatua kero zao mbalimbali na kuongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. Magufuli, itafuta sheria kandamizi zinazowaumiza wananchi.
Sheria hizo ni ile ya kuzuia wananchi wasikate miti ambayo wameipanda wenyewe ili waweze kujikwamua kiuchumi, akisema ni jukumu la mbunge na madiwani wa CCM kuhakikisha sheria zote kandamizi zinafutwa.
"Pia kuna sheria ya kifaa cha kuzimia moto kwenye magari, kimsingi gari nimeinunua mwenyewe, nina bima kwanini nilazimishwe kununua kifaa hicho...nani kawaambia gari yangu itaungua?” alihoji Kinana.
Alisema kuwa inashangaza sheria ya kuzuia kukata miti kuwa na urasimu mwingi ukiwemo wa wananchi kutakiwa kuomba kibali kuanzia ngazi ya kijiji hadi halmashauri na mlolongo mrefu wa kukipata kwake.
Aliwataka wabunge na madiwani ambao watachaguliwa katika uchaguzi ujao, kuhakikisha wanadhibiti michango holela shuleni ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa Taifa.
"Serikali imefuta ada katika shule za msingi na sekondari, lakini walimu wamekuwa wakibuni michango mbalimbali kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo limekuwa likiwakandamiza wazazi," alisema.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Nzega Vijijini, Dk. Hamisi Kigwangala, aliwataka wananchi kuepuka kugawanywa kwa misingi ya dini na ukabila.
Naye Shirima aliwaomba wananchi wa Vunjo kumpa kura nyingi awe mbunge wao ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili akiahidi kuhakikisha wananchi wananufaika na mapato yanayotokana na Mlima Kilimanjaro, kuboresha miundombinu ya elimu, afya na maji.

No comments:

Post a Comment