Wednesday 12 October 2016

WAFUASI CUF KORTINI KWA KUKUTWA NA MABOMU 10



NA FURAHA OMARY

WAFUASI 22 wa Chama cha CUF, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka manne, likiwemo la kukutwa na mabomu ya machozi 10, ambayo yanatumiwa na Jeshi la Polisi.

Pia, washitakiwa hao wanaodaiwa kutenda makosa hayo kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, wanatuhumiwa kuwa wanachama wa kikundi cha ‘Blue Guard’, kinachojitwika mamlaka ya polisi.

Washitakiwa hao ni Hamis Omary Hamis, Said Mohamed Zaharani, Hamid Nassoro au Hemed, Nassoro Humudi Ally, Othuman Humud au Abdallah, Swalehe Ally Swalehe na Hamis Hamis Haji.

Wengine ni Majid Juma, Mohamed Khamis Ally, Ramadhan Juma, Juma Hamad Seif, Masoud Asa Fumu, Jecha Faki Juma, Mbaruku Bakari, Muhsin Ally Juma, Juma Omary Hamis na Haji Rashid Juma.

Pia, wamo  Ally Nassoro au Haji, Ally Juma Salum, Juma Haji au Mmanga, Mohamed Amir Mohamed na Mohamed Zuberi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, aliwasomea washitakiwa hao mashitaka hayo  jana, mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Mwita alidai kati ya Septemba 20 na 25, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na Dar es Salaam, washitakiwa hao na wenzao, ambao hawapo mahakamani, walikula njama ya kutenda kosa kwa kuunda kikosi cha brigadi, ambacho kinafanya kazi kama polisi kinyume cha sheria.

Washitakiwa hao pia wanadaiwa katika tarehe hizo na maeneo hayo, wakiwa wanachama wa kikundi cha ‘Blue Guard’, kwa madhumuni ya kujiingiza katika ajira, walikuwa wakifanya majukumu ya polisi.

Shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Septemba 25, mwaka huu, maeneo ya Mwananyamala ‘A’, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, walikutwa wakimiliki visu vitano na mabomu 10 ya machozi kwa nia ya kuingia kwa jinai.

Washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo pia walikutwa wakimiliki mabomu hayo 10 ya machozi kinyume cha sheria, kwa kuwa kimsingi humilikiwa na Jeshi la Polisi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hao, ambao wanatetewa na Wakili Hekima Yassin, walikana ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Kwa upande wa utetezi, uliwasilisha pingamizi kuhusu shitaka la tatu kwa madai maelezo hayajitoshelezi kwa mujibu wa sheria.

Wakili Yassin alidai shitaka hilo lina upungufu kisheria, hivyo aliiomba mahakama kulitupilia mbali.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mwita alidai pingamizi hilo halina msingi kisheria kwa kuwa shitaka hilo linajitosheleza.

Hati ya mashitaka alidai inasema kwa kifupi mashitaka yanayomkabili mshitakiwa kwa kuwa haiwezi kuweka ushahidi wote.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mwambapa alitoa uamuzi, ambapo alitupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi kwa kuwa halina msingi kisheria.

Pia, Hakimu alitoa masharti ya dhamana baada ya upande wa utetezi kuwasilisha maombi, ambayo hayakupingwa na upande wa jamhuri.

Katika masharti hayo ya dhamana, Hakimu alimtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho, ambao kila mmoja atatia saini dhamana ya sh. milioni mbili.

Washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo walirudishwa rumande hadi Oktoba 20, mwaka huu, kesi itakapofikishwa mahakamani kwa kutajwa.

No comments:

Post a Comment