Sunday 24 September 2017

DIWANI CHADEMA AJIUZULU MBELE YA JPM

DIWANI wa Kata ya Kimandolu, jijini Arusha (CHADEMA), Rayson Ngowi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya Rais Dk. John Magufuli.

Kabla ya Ngowi kujiuzulu nafasi hiyo, alipanda gari moja na Mstahiki Meya wa jiji hilo, Kalisti Lazaro na Katibu wake wa Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, wakati wanaingia katika hafla ya kuwatunuku kamisheni wanajeshi,
iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ngowi alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo muda mfupi baada ya shughuli za kijeshi za kutunuku kamisheni kukamilika, wakati Rais Dk. Magufuli alipotumia nafasi hiyo kuzungumza na wananchi wa mkoa huo.

Wakati akizungumza na wananchi, yaliibuka mabango yaliyobebwa na baadhi ya watu, wakimuomba awapokee wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani, wakiwemo madiwani tisa.

Ngowi alisema aliamua kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na kuchoshwa na karaha mbalimbali zilizopo ndani ya chama hicho, kutoka kwa viongozi, ambao wamekuwa wakishinikiza madiwani kupinga kila jambo hata yale ya maendeleo.

Diwani huyo alisema kujiuzulu kwake siyo kwa shinikizo kutoka kwa mtu yeyote wala kiongozi wa chama chochote, bali ni uamuzi wake binafsi, kutokana na kutambua kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli tangu alipoingia madaraka.

“Ni dhambi kubwa kuendelea kusema kwamba, ninamuunga mkono Rais Magufuli huku nikiendelea kuwa ndani ya CHADEMA, kwa kuwa sitakuwa huru kuonyesha hisia zangu katika kuunga mambo mbalimbali ya maendeleo, kutokana na mtindo wa viongozi wetu kutushinikiza kupinga kila jambo.

“Ni jambo la ajabu na haliwezi kueleweka kamwe kwa mtu aliye mwelewa kusema kwamba, unatukuza Uislamu huku ukiwa Mkristo. Hivyo ili niweze kuutukuza Uislamu barabara, ni lazima nijiunge na Uislamu wenyewe,”alisema.

Akizungumza kuhusu tukio hilo,  Rais Magufuli alisema maendeleo hayana chama na  aliwapokea madiwani hao kwa moyo mmoja na kuongeza kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni taasisi kubwa, hivyo hawatakosa mahali pa kusaidia.

Dk. Magufuli alisema iwapo uchaguzi utatangazwa upya katika kata walizotoka, hakutakuwa na haja ya kutafuta wagombea wengine, bali waliojiuzulu nafasi zao watapewa nafasi ya kugombea kwa tiketi ya CCM, kwa kuwa wana uwezo, isipokuwa walichukizwa na baadhi ya mambo kama walivyoyataja wenyewe.

Madiwani wengine waliopokelewa, kata zao zikiwa kwenye mabano ni Andrew Sikawa (Leguruki), Solomon Laizer (Ngabobo), Emmanuel Mollel (Makiba), Japhet Jackson (Ambureni), Josephine Mshili (Viti Maalumu) na  Bryason Issangya (Maroroni).

Wengine ni Goodluck Kimario, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Machame Magharibi na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Evarist Kimathi, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mnadani, Abdallah Chiwili (Weruweru) na Credo Kifukwe (Muriet).

Mbali na madiwani hao, wengine ni Mosses Kaaya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwausoro, Kata ya Maroroni, Sarikiaeli Kaaya (Mshauri wa CHADEMA), Samwel Solomon (Kiongozi wa M4C ) na Abrahan Kaaya  (Katibu Mwenezi Wilaya ya Meru).

No comments:

Post a Comment