Sunday 24 September 2017

DK. MPANGO ASHTUKIA MCHEZO MCHAFU TRA


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufanya mabadiliko makubwa ya watumishi walioko katika Idara ya Upimaji na Ukaguzi wa Mizigo, baada ya kubaini baadhi yao wanajihusisha kwa namna moja au nyingine na upotevu wa mapato ya serikali.

Pia, Dk. Mpango ametoa muda wa siku saba kwa TRA, kumpa taarifa kamili ya utekelezaji wa maagizo hayo, ikiwemo kuwahamisha watumishi wote waliokaa muda mrefu kwenye eneo hilo la upimaji na ukaguzi wa mizigo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato ya serikali katika bandari hiyo.

Dk. Mpango alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, alipofanya ziara ya kushitukiza katika Kituo cha Forodha Bandarini, kilichoko katika Bandari ya Dar es Salaam.

Waziri huyo alishangazwa na kitendo cha mapato katika bandari hiyo kutokuongezeka, licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali, kuiboresha kutokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanaoshirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi ya serikali.

“Pamoja na kuwepo kwa mitambo ya kukagua mizigo (Scanners), baadhi ya bidhaa zinakadiriwa kodi ndogo, ikilinganishwa na thamani ya mizigo huku mizigo mingine ikiwa siyo ile iliyotajwa kuwemo kwenye makontena na hupitishwa na watumishi wasio waaminifu,” alisisitiza.

Dk. Mpango aliuagiza uongozi wa TRA, kuhakikisha unaongeza mapato katika bandari ya majahazi, kutoka wastani wa mapato ya sh. bilioni 3.5, kwa mwezi hadi sh. bilioni tano, kulingana na malengo yaliyowekwa baada ya kubainika kuwa, kuna ukwepaji mkubwa wa mapato ya serikali katika eneo hilo.

Dk. Mpango aliuambia uongozi wa TRA, kuhakikisha kuwa Bandari ya Majahazi ianze mara moja kutumia mfumo wa kukusanya mapato ujulikanao kama TANSIS, ili kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

Pia, aliviagiza vyombo vya dola kuwachunguza watumishi wote, wakiwemo wa ngazi za juu katika idara ya forodha bandarini na kuwachukulia hatua kali wale watakaobainika kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoikosesha serikali mapato.

No comments:

Post a Comment