Monday 25 September 2017

SERIKALI YAPIGA 'STOP' MATIBABU NJE YA NCHI




WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesisitiza udhibiti wa rufaa zisizokuwa za lazima kwa wagonjwa kutibiwa nje ya nchi, bila kujali wadhifa, cheo au umaarufu wa mtu.
Wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wametakiwa kuhakikisha matibabu yanayowezekana kufanyika katika hospitali hiyo, yafanywe bila kujali wadhifa wa mtu yeyote.
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alisema hayo jana, alipozindua vyumba vya upasuaji kwa watoto, ambavyo vimegharimu Dola za Marekani 675,000 (Sawa na sh. bilioni 1.5) katika Hospitali ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, serikali inaridhishwa na kasi ya utoaji huduma katika Hospitali ya Muhimbili, ikiwa ni pamoja na kutekeleza jitihada za serikali ya awamu ya tano ya utoaji wa huduma bora kwa Watanzania na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi.
“Ni dhahiri kuwa, ili nia hiyo iweze kutekelezeka, ni muhimu kuwekeza katika kuboresha miundombinu na kununua vifaa vya kisasa pamoja na kuwa na wataalamu wa kutosha wenye weledi wa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Waziri Ummy aliwasihi wataalamu kusimamia misingi ya taaluma zao katika kufanya maamuzi wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Aliwasihi kuvitunza vifaa vilivyofungwa kwenye vyumba hivyo vya upasuaji na kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Maseru, alisema msaada huo umetoka shirika lisilo la kiserikali la Archie Wood Foundation la Uingereza.
Alisema vyumba hivyo vitawezesha watoto kufanyiwa upasuaji mara 10, kwa wiki, badala ya mara tatu kama ilivyokuwa awali.
Alisema hiyo itaondoa kero kwa watoto waliokuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata huduma hiyo.
Mshauri Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto, Profesa George Youngson kutoka Archie Wood Foundation, alisema wataendelea kuunga mkono jitihada za serikali kupitia MHN, katika kutoa huduma za ubingwa wa hali ya juu ili kupunguza rufaa zisizokuwa za lazima.
Alisema watahakikisha wanatoa msaada wa vifaa tiba, ikiwezekana  kuleta wataalamu nchini kufanya upasuaji mgumu.

No comments:

Post a Comment