Tuesday, 31 May 2016
SMS: WANAOHAMASISHA UBAGUZI KUSHUGHULIKIWA
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema uvumilivu katika vitendo vya kibaguzi na hujuma, vinavyofanyika Pemba kwa misingi ya itikadi za kisiasa, sasa vimefikia kikomo na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wanaohamasisha matukio hayo.
Hayo yalisemwa jana na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, wakati akiwasilisha Makadirio Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2016/2017, katika Baraza la Wawakilishi.
Balozi Seif alisema vitendo hivyo vinakwenda kinyume na misingi ya utu na ubinadamu pamoja na utawala bora na haviwezi tena kuvumiliwa na kuachwa kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa jamii.
"Serikali ya Mapinduzi imechoshwa na matukio ya vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa kwa malengo ya kisiasa na kusisitiza kwamba imetosha, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao," alisema.
Aliyataja matukio yanayofanyika, yakilenga kuathiri huduma za kijamii na uchumi ni kuchomwa moto kwa mashamba ya mikarafuu huko Pemba.
Aidha, alisema wananchi wamekuwa wakigomewa katika kupata huduma za kijamii, ikiwemo bidhaa za chakula kwa sababu tu ni waafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Inasikitisha sana kuona mtu anachomewa shamba lake la mikarafuu, sasa kwa faida ya nani? Eti kwa sababu ni mfuasi wa CCM ? Jambo hili sisi hatukubaliani nalo,"alisema.
Aliwataka watendaji, wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya, kusimamia amani na utulivu na kamwe wasisite kuwachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
"Watendaji wa serikali, wakuu wa mikoa na wilaya katika sehemu zenu, msikubali kuruhusu vitendo vya aina hiyo kwa watu wengine kuonewa kwa makusudi," alisisitiza.
Akizungumzia suala la matumizi ya dawa za kulevya, Balozi Iddi alisema hilo ni janga la kitaifa na hatua za kudhibiti uingizaji wake inatakiwa kudhibitiwa kwa kuweka mikakati ya hali ya juu.
"Tumejizatiti kupambana na tatizo la uingizaji wa dawa za kulevya, ambapo tumeweka mkazo kudhibiti maeneo ya uwanja wa ndege na bandari ya Malindi," alisema.
Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika kupambana na tatizo hilo, ikiwemo wahalifu kutumia bandari bubu zilizoko katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Alisema hawalifu wamekuwa wakizitumia bandari zisizo rasmi kwa ajili ya kuingiza dawa za kulevya.
"Zipo changamoto mbalimbali katika suala zima la kupambana na madawa ya kulevya kutokana na kuwepo kwa bandari, ambazo sio rasmi zilizoko mpaka vijijini," alisema Balozi Iddi.
Kuhusu uchaguzi wa marudio, aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kujitokeza kwa wingi na hatimaye kufanikisha uchaguzi huo kuwa wa kidemokrasia.
Alisema katika kufanikisha uchaguzi huru na haki, sheria ya tume ya uchaguzi ya mwaka 1985, itafanyiwa marekebisho kwa lengo la kuleta ufanisi wa kazi.
"Sheria Na.11 inayounda Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), itafanyiwa marekebisho kwa lengo la kuleta ufanisi kwa watendaji wa tume kusimamia uchaguzi huru na haki," alisema.
Balozi Seif aliliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya sh. bilioni 5,992,076,000, kwa mwaka wa fedha 2016-2017.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment