Tuesday 22 September 2015

DK. SHEIN: CCM HAINA MBADALA





NA MOHAMMED ISSA, BUNGI- ZANZIBAR

MGOMBEA urais wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema CCM ina uwezo mkubwa wa kuongoza nchi na kuwa hakuna mbadala wa CCM.
Amesema CCM itaendelea kubaki kuwa CCM na itaendelea kuongoza serikali kutokana na kuwa na  uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi.
Dk. Shein alisema muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa, haukuja kwa lengo la kuleta vurugu na uvunjifu wa amani bali ulikuja kuleta maridhiano na mshikamano kwa wananchi.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, kumeibuka vikundi vyenye lengo la kuvuruga uvunjifu wa amani na kuwagawa wananchi,  hivyo aliwataka wananchi wasikubali kugawanywa na watu wasioitakia mema Zanzibar.
Aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika uwanja wa mpira Bungi Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini, Unguja na kuhudhuriwa na maelfu ya wana CCM na wananchi.
“Tuna uwezo mkubwa wa kuongaza nchi, hivyo hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi zaidi ya CCM, ninawaomba muendelee kutuamini kwa kutupa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu,” alisema.
Alisema anaamini kuwa ataendelea kuwa Rais wa Zanzibar, kutokana na mambo mengi aliyofanya visiwani humo.
Mgombea huyo akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, alisema iliyopita imetekelezwa kwa asilimia kubwa na hivi sasa Zanzibar, imepiga hatua ya maendeleo yakiwemo ya kiuchumi, kijamii na miundombinu.
Alisema huduma za maji zimeongezeka katika Mkoa wa Kusini Unguja na kufikia asilimia 76.6 ya upatikanaji wa huduma hiyo ambapo Mkoa wa Mjini Magharibi umefikia zaidi ya asilimia 86.
Dk. Shein alisema katika miaka mitano ya utawala wake, amefanikiwa kujenga mtandao wa barabara Unguja na Pemba wenye zaidi ya kilomita 120, ambazo hivi sasa zinapitika kwa uhakika.
Kuhusu sekta ya kilimo alisema kinachangia kwa asilimia 31 ya pato la taifa, hivyo serikali yake itaendelea kuiboresha sekta hiyo.
Alisema mwaka jana na mwaka huu, wamevuna tani zaidi ya 600,000  za kilimo na mafanikio hayo yametokana na kuwepo kwa zana bora za kilimo.
Dk. Shein alisema nia ya serikali ni kupunguza kuagiza mchele kutoka nje ya nchi na kwamba ifikapo mwaka 2018, watafanikiwa kwa zaidi ya asilimia 60.
“Mafanikio yote haya yametokana na juhudi kubwa ya serikali na juhudi zangu na za Chama changu hivyo asitokee mtu yoyote akadai yametokana na yeye,” alisema.
Dk. Shein alisema sekta ya afya imeimarishwa kwa kiasi kikubwa ambapo vituo vya afya vimeongezwa Unguja na Pemba.
 Balozi Amina Salumu Ali, alisema wananchi wana kila sababu ya kumchagua Dk. Shein, kutokana na mambo mengi aliyofanya katika autawala wake.
Aliwataka wananchi wasikubali kudanganywa na wapinzani badala yake wahakikishe wanakirudisha Chama madarakani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Shamsi Vuai Nahodha, alisema mgombea urais wa chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa Waziri Kiongozi kwa miaka mine, lakini alishindwa kuibadilisha Zanzibar, sasa atawezaje kuibadilisha nchi hiyo kwa siku 100.
Alisema mwaka 2010 hadi sasa, Maalim Seif, alishika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, lakini ameshindwa kutoa ushauri mzuri ndani ya serikali hivyo aliwataka wananchi wasikubali kudanganywa na mgombea huyo.
Shamsi ambaye ni Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, alisema serikali imefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja kujenga Chuo Kikuu cha Zanzibar, imefanimkiwa kupambana na malaria, kujenga miundombinu ya barabara na maji na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Balozi Seif Ali Iddi, alisema Maalim Seif ameishiwa sera na hivi sasa kazi yake ni kueneza uongo kwa wananchi.
Aliwataka wananchi wasikubali maneno ya uongo wanayoambiwa na Maalim Seif kwani hana uwezo wa kuongoza nchi.
Balozi Idi aliwaomba wananchi watulie na wasiwe na wasi kwani CCM itashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Alizitaja sababu ya Chama kupata ushindi kuwa ni pamoja na haijawahi kushindwa, sababu ya kushinda wanayo na mambo mengi Chama kimefanya.
Hata hivyo, alisema anashangazwa kuona wapinzani wanataka kujenga ICU Ikulu kutokana na kusimamisha wagombea ambao ni wagonjwa.
“Mwaka huu tumeshuhudia vioja…mwaka huu, wapinzani wanataka kuigeuza ikulu kuwa wodi ya ICU kwani Tanzania Bara wamesimamisha mgonjwa na hapa Zanzibar, mgombea mwenyewe kila sehemu ana viraka,” alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema msingi wa kuingia kwenye uchaguzi ni ilani ya uchaguzi ambayo tayari CCM, imeshaizundua wakati wa uzinduzi wa kampeni za urais.
Alisema Maalim Seif na wenzake walizindua kampeni zao bila ya kuwa na ilani ya uchaguzi na kwamba hana jipya ambalo anaweza kulifanya.
“Maalim Seif ameingia kwenye uchaguzi bila ya ilani  sijui hiyo serikali ataiongoza vipi,” alihoji.
Vuai alisema baada ya kuona ameingia kwenye uchaguzi bila ya ilani ya uchaguzi, Maalim alizindua ilani yake juzi ambayo ina kurasa 94 na kwamba mambo mengi yameyakopiwa kutoka kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ina kurasa zaidi ya 236.
Alisema Ilani ya CCM ina sura nane ambazo kila sura imeelezea mambo ya maendeleo na katika ilani hiyo ya Chama sura ya kwanza inaelezea masuala ya uchumi na maendeleo.
Vuai alisema nchi zote duniani huwezi kuwa na maendeleo bila ya amani, uchumi imara, hivyo ipo haja ya kudumisha Muungano wa Tanzania.
Aliwataka wananchi wakiunge mkono Chama kutokana na sera mzuri na kudumisha amani iliyopo hapa nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Unguja ambao walifika katika viwanja hivyo kuanzia saa nne, asubuhi wakiwa na sare za Chama.

No comments:

Post a Comment