Tuesday 22 September 2015

BALOZI SEIF: TUMEGUNDUA JANJA YA MAALIM SEIF


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Ali iddi amesema  CCM imegundua kuwa upotoshaji anaoufanya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif katika mikutano yake ya kampeni ni janja yake ya kujaribu kuwapa moyo wanachama na wafuasi wa chama hicho ambao tayari wameonesha kukata tamaa.

Balozi Seif ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano wakampe ni huko Bungi Wilaya Kati kuwa Maalim Seif ambaye ni mgombea urais kupitia chama cha CUF hana kipya cha kuwaeleza wafuasi wake hivyo analofanya hivi sasa kila akisimama majukwani ni kusema uongo ili kujaribu kuwapa moyo baada kuona wamekata tamaa na ushindi.

“Maalim acha kuwadanganya wanachama na wafuasi wako, CCM hawadanganyiki na ghiliba zako mwaka huu ndio mwaka wa kuizika CUF”alielezaBalozi Seif.

Balozi Seif alisema Maalim Seif na CUF yake hawana sifa za kuongoza na kuwataka wasahau kuingiaIkulu.

“Nia ya kushinda tunayo, hatujawahi kushindwa, dhamira ya kushinda tunayo na sababu za kushinda tunazo”alisisitiza Balozi Seif.


 VUAI: CUF IMECHEMSHA, HAINA ILANI
Chama cha Wananchi-CUF kuzindua kampeni za uchaguzi bila ya Ilani ni kielelezo tosha kuwa chama hicho kimekosa umakini wa uongozi hivyo hakipaswi kupewa fursa ya kuongoza nchi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni uliofanyika Bungi Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini kuwa chama cha CUF baada ya kuoneshewa kidole na baadhi ya wananchi kwa kukosa Ilani harakaharaka kilikurupuka na kuandaa Ilani na kuizindua juzi.

Matokeo ya kukurupuka huko Vuai alibainisha kuwa chama hicho kimejikuta kikinakili Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kubadilibadili kurasa tu.

Alifafanua kuwa vyama makini kwa uongozi vimekuwa vikiandaa Ilani zake zinazogusa kila sehemu ya maisha ya mwananchi wakati wa chaguzi zote kama ilivyofanya Afro Shirazi wakati wa chaguzi za kutafuta Uhuru hadi hivi sasa CCM kuendeleza nchi. Ilani hizo ndio zinazowavutia wananchi na kukichagua CCM kushika dola wakati wote.

Ilani ya ASP katika mkutano wa mwisho wa kampeni uliofanyika Kisiwandui Unguja ilieleza kuwa elimu na matibabu itatolewa bure na ndio maana ilishinda uchaguzi japoku walifanyiwa ghiliba na kunyimwa kuongoza nchi.


SHAMSI:MAALIM SEIF HANA DHAMIRA WALA NIA YA KUINDELEZA ZANZIBAR

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Shamsi Vuai Nahodha amesema Maalim Seif Sharif Hamad hana dhamira wala nia ya kuindeleza Zanzibar na kwamba kauliza kuibadili Zanzibar ndani ya siku mia moja endapo atakuwa Rais ni ghiliba za kisiasa tu kupata kura.

Alifafanua kuwa miaka tisa ya Maalim Seif kuwa katika madaraka makubwa kwa nyakati tofauti katika Serikali ya Zanzibar ameshindwa kuleta mbinu au mpango wa kuifanya  Zanzibar kama nchi ya Singapore.

“Alikuwa Waziri Kiongozi kwa miaka 4 huku akipewa mamlaka makubwa na Rais wa wakati huo marehemu Mzee Abdulwakil na baadae hivi sasa miaka mitano akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais hajafanya lolote”Alieleza Shamsi na kusisitiza kuwa kama miaka tisa ameshindwa ataweza siku mia moja.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alieleza kuwa inaonesha kiongozi huyo anazeeka vibaya kwa kuwa hata huo uumini wake wa demokrasia una mashaka kwa kuwa yeye mwenyewe anashindwa kutekeleza.

“Mbona kama ni muumini wa demokrasi ya Uingereza mbona haifuati? Mbona wenzake wakishindwa uchaguzi mara moja tu hujiuzulu lakini yeye anashindwa uchaguzi anaendelea kung’ang’ania” alisisitiza Shamsi.

Aliwaeleza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa kiongozi huyo ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais kupita akiwaeleza wananchi kuwa serikali haijafanya kitu zote hizo ni ghiliba ambazo wananchi wanapaswa kuwa makini na kutompa nafasi yoyote yeye na chama chake.

No comments:

Post a Comment