Tuesday 22 September 2015
DK. SHEIN AAHIDI KUJENGA HOSPITALI MPYA BINGUNI
MGOMBEA nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameahidi kujengwa kwa hospitali mpya na ya kisasa huko Binguni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika Bungi Miembe Mingi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja uliohudhuriwa na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema kuwa hospitali hiyo itakuwa kubwa na ya kisasa, ambayo itakuwa na Idara mbali mbali zikiwemo Idara ya upasuaji wa moyo, haja ndogo, saratani kwa lengo la kupunguza mzigo katika hospitali ya Mnazi Mmoja na kuwataka wananchi kuilinda ardhi hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali hivi sasa inatafuta Fedha kwa ajili ya ujenzi huo huku akieleza kuwa taratibu kadhaa za awali zimeshafanyika na kuwapongeza wananchi wa Wilaya ya Kati kwa ustahamilivu wao kwa kuwa Wilaya hiyo bado haijapa hospitali kubwa.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kueleza kuwa wapo wanaoyabeza Mapinduzi hayo bila ya kutambua kuwa ndiyo yaliyowakomboa watu wa Zanzibar wakiwemo wakwezi, wakulima, wavuvi na wengine wote.
Akisema kuwa Mapinduzi ndiyo yaliyoleta muelekeo na kueleza kuwa wale wanaojifanya mahodari wa kusema kama si hayo Mapinduzi uwezo huo wasingeliupata.
Aliwataka wananchi na wanaCCM kuzingatia hilo na kuwaeleza kuwa wasijaribu watu wa kuwapa uongozi na badala yake waipe CCM kuongoza nchi.
Alisisitiza kuwa hakuna mbadala wa CCM na kwamba kama CCM isingetaka vyama vingi visingekuwepoa kwani iliamua kwa Katiba zake zote mbili kwa maslahi ya maendeleo na lengo la kusimamisha demokrasia.
Alisema kuwa yeye anaamini sana kuwa wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar wanaojua uchungu wa nchi hii na wanaotaka maendeleo wataichagua CCM na kusema kuwa chama hicho kina uwezo wa kuongoza nchi.
Dk. Shein alisema kuwa bado Zanzibar inahitaji watu wenye uwezo wa kuiletea maendeleo na kusisitiza kuwa hakuna mbadala waCCM.
Akieleza juu ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa alisema kuwa asilimia 66 wa wananchi wa Zanzibar waliridhia kuwepo kwa Serikali hiyo na kueleza kuwa Mfumo huo haukuja kuleta vurugu na uhasama, kutukanana, wagombane wala kudharauliana.
Alisisitiza kuwa madhununi ya Serikali hiyo ni kuwa na Serikali ya pamoja na kusaidiana katika kuleta maendeleo huku akieleza jinsi ya baadhi ya vikundi vya kuvuruga amani vilivyojitokeza ndani ya mwaka mmoja na nusu tu baada ya kuanza kazi Serikali hiyo.
Dk. Shein alisema kuwa mwenendo na mfumo wa Zanzibar uliwekwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na mashujaa wenzake na baada ya hapo utaratibu huo umekuwa ukifuatwa kwa kasi na kwa malengo yale yale ya kuleta maendeleo.
Alisema kuwa watu wote wa Zanzibar wamekuwa sawa katika Serikali ya Awamu ya kwanza na Awamu zote zilizofuata sambamba na kuwakumbusha wananchi kuwa tangu wakati wa ASP na hatimae CCM walijua kuwepo kwa Ilani ya uchaguzi ni jambo muhimu sana na ndipo walipozitengeneza.
Alisema kuwa yote yalioahidikwa katika Ilani za CCM, kwa lengo la kufanywa yametekelezwa na kusisitiza kuwa wananchi wataichagua CCM na yeye atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi huku akiahidi kufanya mengi kama yalivyotangulia kufanywa na chama hicho.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na CCM iliahidi kuondoa kero na katika mambo yalioahidiwa na kufanywa kwa asilimia 90 ni suala la uwekaji wa msingi wa maji safi na salama nchini.
Alisema kuwa katika Jimbo lililokuwa na matatizo makubwa ya maji ni Tunguu, na kueleza kuwa juhudi kubwa zimefanywa katika kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi na hivi sasa huduma hiyo imekuwa ikipatikana.
Alisema kuwa tatizo la mahitaji ya maji, hayazungumzwi tena katika Wilaya ya Kati wala Kusini, na hatua za maji Unguja na Pemba zimechukuliwa.
Dk. Shein alisema kuwa miji ya Wete, Chake, Mkoani na Wilaya ya Kati Zanzibar hali ya maji imeimarika, na kueleza kuwa kipindi kijacho nguvu zitaongezwa zaidi ili kufikia asilimia 95.
Alisema kuwa ahadi zilitolewa na CCM katika kuimarisha miundombinu ya barabara zimetekelezwa huku akieleza umuhimu wa kujenga barabara katika sehemu za kilimo tofauti na watu wengine wanavyodharau juhudi hizo.
Dk. Shein aliahidi kuwa Barabara inayokwenda Jozani hadi Charawe na Jozani kwenda Ukongoroni imejengwa kwa hatua za kifusi na katika kipindi kijacho cha miaka mitano zitatiwa lami.
Aidha, aliahidi kuwa barabara ya Umbuji hadi Uroa itajengwa kwa kiwango cha lami hayo ndio mambo ambayo tayari yamo katika Ilani ya CCM.Aliongeza kuwa maeneo mengi ya Wilaya ya Kati ni maeneo ya kilimo hivyo sekta hiyo nayo itaimarisha sambamba na wakulima kuendelea kusaidiwa.
Alisema kuwa mambo 12 ya msingi yamefanywa yakiwa pamoja na kutafuta masoko, mashamba darasa 1200, ukuaji wa mavuno ya mpunga pamoja na juhudi nyengine za kuimarisha sekta hiyo ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuungwa mkono na nchi marafiki na washirika wa maendeleo zikiwemo China na Korea.
Kwa upande wa zao la karafuu, Dk. Shein alisema kuwa mipango aliyoifanya katika zao la karafuu ni mikubwa na asitokee mtu kujisifu kuwa kafanya yeye bali ni Serikali chini ya uongiozi wake. "Wengine wanataka sifa tu..”,alisema Dk. Shein
Tuliamua Serikali kuwapa fidia wakulima, dawa za kuulia wadudu, mbolea, mbegu na mambo mengineyo na kusema kuwa ipo haja ya kuwasifu wakulima.
Dk. Shein alisema kuwa Wanachi wa Tunguu wamebahatika kuwa na Chuo Kikuu katika Jimbo hilo na kueleza kuwa Chuo hicho kitaimarishwa.
Aliendelea kueleza suala la elimu kuendelea kuwa bure, kwa Msingi na Sekondari, na kusema kuwa kutokana na uchumi kwenda vizuri na nia yake aliyonayo hilo litawezekana.
Alieleza kuwa hatua zinachukuliwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikwia ni pamoja na uchimbaji wa mafuta na kupinga kauli za kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore kwa siku 100.
Alisema kuwa nchi itajengwa kwa uwezo uliopo, na na Serikali chini ya uongozi wa CCM imejiandaa kwamba Zanzibar ikifika mwaka 2020 makusanyo yatakuwa Bilioni 800 kwa mwaka na kueleza kuwa baada ya miaka yake mitano ya uongozi makusanyo hivi sasa ni Bil 40.5 kwa mwaka, hivyo kwa kasi ya Ilani na kuzingatia hatua za miundombinu iliyowekwa Bandari ya Mapigaduri itajengwa.
Alieleza pia, juhudi zinazofanywa katika ujenzi wa jengo la uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Dk. Shein, aliomba kura kwa wananchi na wanaCCM wote, Magufuli, Samia, Wabunge na WawakilishiTunguu, Chwaka na Uzini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment