Saturday, 27 August 2016
SPIKA MSTAAFU MSEKWA AFUNGUKA
SPIKA wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa, amewaasa Watanzania kuacha kufuata mkumbo wa kisiasa, badala yake watii mamlaka ili kuepuka uvunjifu wa sheria unaoweza kusababisha madhara kwa taifa.
Msekwa aliyasema hayo jana, Dar es Salaam, wakati akizungumzia mwenendo wa kisiasa wa hapa nchini na utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais Dk. John Magufuli.
Alisema lipo tatizo la watu wengi kufuata mkumbo katika mambo mbalimbali bila ya kuchunguza na kufahamu ukweli wa jambo husika.
“Ni hulka ya Watanzania kushabikia mambo wasiyoyafahamu, ilimradi tu yanawafurahisha masikioni au machoni mwao. Unaweza kuangalia hata mitaani, watu hukimbilia ngoma bila ya kujua inatoka wapi na inakwenda wapi. Nawasihi wananchi kuwa makini na mbinu za siasa zinazotumiwa na baadhi ya vyama kwa kuwa nyingine zina madhara kwa jamii,”alisema.
Akifafanua mwenendo wa kisiasa hapa nchini, Msekwa alisema bado wanasiasa wengi hawafuati kanuni za ushindani wa kisiasa katika kutafuta madaraka, badala yake wanatumia mbinu zinazovunja sheria za nchi na hatimaye kupambana na mamlaka.
“Ushindani wa kisiasa ni jambo la kawaida na linalokubalika, ingawa ni lazima ufuate sheria, kanuni na utaratibu uliowekwa ili kufikia lengo, hivyo kubuni vitu vinavyochochea utovu wa nidhamu na uvunjifu wa amani sio jambo zuri,"alisema.
Spika mstaafu Msekwa alisema utendaji wa Rais Dk. Magufuli ni wa kuridhisha na wa aina yake kwa kuwa amekusudia kuleta mabadiliko chanya kwa Watanzania na kuondoa mfumo wa utendaji kazi kwa mazoea, jambo ambalo limesaidia kurudisha nidhamu kwa watumishi wa serikali.
Akizungumzia uzoefu wake katika masuala ya kuongoza bunge, alisema bunge la zamani lilikuwa na nidhamu kubwa na kuheshimika, na kulikosoa bunge la sasa kwa kutozingatia hayo.
Alisema tangu zamani, wapinzani kazi yao kubwa ni kuipinga serikali iliyo madarakani, lakini kwenye bunge aliloliongoza, walikuwa wakipinga kwa kutumia hoja na kufuata kanuni bila ya kudharau mamlaka ya Spika wala serikali iliyo madarakani.
“Kanuni zinatoa nafasi kwa mbunge asiyeridhika na uamuzi wa Spika, kushitaki kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge na kamati hiyo itasikiliza na kutoa uamuzi kama inavyofanyika mahakamani, lakini wabunge wa sasa hawataki kutumia utaratibu, bali hutumia mbinu tofauti ili waweze kupata sifa, ambazo hazina tija kwa wananchi waliowachagua,”alisema.
Msekwa pia ameviasa vyama vya upinzani kutumia mbinu nzuri katika kutafuta madaraka bila ya kuvunja sheria au kuhatarisha amani ya nchi kwa kuwa wananchi waliowachagua, wanategemea matokeo ya kazi waliyoahidi kuifanya badala ya kujikita katika malumbano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment