Monday 6 June 2016

DIANA CHILOLO ATAKA SHAKA AKABIDHIWE RASMI MIKOBA

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Diana Chilolo, amesema wakati umefika kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, kukabidhiwa rasmi mikoba ya kuiongoza jumuia hiyo.

Alisema amekuwa akifuatilia kazi, ziara na maelekezo ya Shaka kwa jumuia yake na kuonyesha wazi kwamba, amekomaa na anatosha kushika wadhifa huo.

Diana alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha ndani cha CCM, kilichowashirikisha viogozi wa Kamati ya Siasa ya CCM na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Singida, iliyofanyika kwenye ofsi za Chama mkoani hapa.

Alisema Shaka ni kiongozi anayejituma na kujitambua kutokana na utendaji wake ndani ya muda mfupi, tangu alipokaimishwa nafasi hiyo.

"Wanapochomoza vijana kama Shaka, Chama kinapata matumaini zaidi kuwa hata kama wazee ndani ya Chama wataishiwa nguvu za kupambana, wapo watu wa kukitetea na kukiendeleza kwamba uhai wa CCM utatabaki imara,"alisema.

Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu kutoka mkoa wa Singida kwa vipindi vitatu, aliwataka vijana wengine kufuata nyayo za Shaka na kuiga ujasiri na uthubutu wake kwa sababu sifa ya kiongozi ni kutenda, kubuni na kuendeleza mambo ya manufaa.

"Nikiwa Mjumbe wa NEC, sitaona muhali au fedheha kumsemea Shaka kama anafaa kukabidhiwa jumuia yetu. Nina ushahidi wa uchapakazi wake na heshima mpya mliyonayo sasa UVCCM," alisema.

Katika kikao hicho, Shaka aliwataka watendaji wa jumuia hiyo kuendelea kuwa karibu na viogozi wa Chama kwa lengo la kujifunza, kuelimishwa na kukomozwa kiakili na imani ya siasa ya CCM.

No comments:

Post a Comment