Monday 6 June 2016

TRA YAKUSANYA TRILIONI 1.032

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imevuka lengo la kukusanya mapato yake kwa mwezi Mei, mwaka huu, kwa kukusanya sh.trilioni 1.032, wakati lengo lilikuwa ni kukusanya sh.trilioni 1.025.

Hayo yalielezwa jana na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa, kuhusu mwenendo wa makusanyo ya mapato.

Alisema mamlaka hiyo inaendelea na jitihada mbalimbali ili kuhakikisha inafikia na kuvuka lengo la makusanyo yaliyopangwa na serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016.

Kidata alisema malengo ya makusanyo yaliyowekwa na serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/16, ni shilingi trilioni 12.054, na hadi sasa wameshakusanya shilingi trilioni 11.956, sawa na asilimia 99.2 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

"Katika kuhakikisha kuwa tunafikia lengo la serikali au kuvuka kabisa, kwa mwezi mmoja uliobaki, TRA tumejiwekea mikakati thabiti ya kuongeza mapato na tumeendelea kupambana na magendo, hususani katika pwani ya bahari ya Hindi na mipaka yote. Lengo ni kupambana na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na wanaokiuka kutumia mashine za kozi za kielektroniki," alisema Kidata.

Alisema katika kuhakikisha kuwa wanafikia lengo hilo, wamepanga kuwawajibisha wafanyakazi wa mamlaka hiyo wasio waadilifu pamoja na kuhakikisha wanaboresha zaidi mifumo itakayompa urahisi mlipakodi katika zoezi la ulipaji kodi wa hiari.

Katika hatua nyingine, Kamishna Mkuu huyo alisema kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli na kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa ushirikiano katika matumizi ya mashine za EFD, mamlaka hiyo imeanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ugawaji wa mashine hizo kwa wafanyabiashara wadogo kwa mkoa wa Dar es salaam.

"Tumeshaanza kugawa mashine za EFD kwa wafanyabiashara wadogo na kwa kuanzia, tumeanza na mkoa wa Dar es salaam, ambapo wafanyabiashara 5,703, wenye mauzo ghafi kati ya shilingi milioni 14 na milioni 20, kwa mwaka, tumeshaanza kuwapatia. Zoezi hilo lilianza Juni Mosi, mwaka huu," alisema.

Kwa mujibu wa Kidata, zoezi hilo litaendelea katika mikoa yote ya Tanzania, ambapo hadi ifikapo Disemba, mwaka huu, wafanyabiashara wote watakuwa wameshapatiwa. Alisema
jumla ya mashine laki mbili zinatarajiwa kutolewa kwa wafanyabiashara.

No comments:

Post a Comment