Monday 6 June 2016

WANAOAJIRI WAGENI BILA KUTOA TAARIFA KUKIONA CHA MOTO


SERIKALI imetangaza vita dhidi ya kampuni zinazoajiri wageni na kushindwa kuwasilisha taarifa na orodha ya wafanyakazi hao kwa mujibu wa sheria.

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika ukiukwaji wa sheria inayowataka kuwasilisha orodha na taarifa za maendeleo ya wageni hao.

Akizungumza Dar es Saalam, jana, Kaimu Kamishna wa Utawala na Fedha wa Idara ya Uhamiaji, Abbas Irovye, alisema kanuni za serikali ya Tanzania zinawataka raia wote wanaoingia nchini kwa ajili ya ajira, kuwa na vibali halali vya kazi na makazi ili kuwatambua.

Alisema sheria inawataka kila baada ya robo tatu ya mwaka, kutoa taarifa za wageni hao ili serikali iwatambue katika shughuli zao za uzalishaji.

"Raia mgeni anapopata ajira hapa nchini, kampuni husika inapaswa kutimiza masharti ya kupata kibali cha kazi hiyo, ambayo yameratibiwa na serikali,"alisema.

Kwa mujibu wa kamishna huyo, zipo baadhi ya kampuni zimeomba vibali vya kazi kwa wageni na kuanza kazi mara moja, kinyume na inavyotakiwa, ambapo anatakiwa kuomba tena kibali cha ukazi.

"Baada ya kupata vibali hivyo vya kazi na ukazi, ndipo unatakiwa kuanza kazi kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza,"alisema.

Alisema sheria namba nane, iliyopitishwa na bunge mwaka jana, iliongezewa baadhi ya adhabu katika suala hilo, ambapo adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka miwili jela.

Kamishna huyo alisema kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi April, mwaka huu, wageni waliokamatwa kwa makosa ya uhamiaji ni 4,792.

Irovye alisema kwa mwezi Januari, wageni 1,467 wakikamatwa, Februari wageni 997, Machi wageni 1,771 na Aprili wageni 557 na kwamba, wageni 1,796 walifukuzwa nchini kwa makosa hayo huku 1,417 wakifikishwa mahakamani.

"Waliofungwa kwa makosa hayo ni 132, kesi zinazoendelea mahakamani ni 383 na waliolipa faini ni 388. Jumla ya kesi 509 zinaendelea kusikilizwa kwa kukosa ushahidi,"alisema.

Alisema serikali inawatambua wageni 7,441, ambao wamewasilisha maombi ya vibali vya ukazi, kati yao 3,495 wamefuata sheria ya maombi hayo.

"Idadi ya wageni 3,998 ndio wamelipia pesa za vibali vya maombi ya ukazi kwa mujibu wa sheria na kuzingatia taratibu na kanuni za serikali ya Tanzania,"alisema.

Alisema kwa kipindi hiki cha miezi minne, Idara ya Uhamiaji imefanikiwa kuongeza maduhuli (mapato) ya ukusanyaji wa tozo za makosa ya masuala ya uhamiaji.

No comments:

Post a Comment