Monday 6 June 2016

DK. SHEIN ATOA ONYO KALI KWA WAFANYABIASHARA


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga kuwafuatilia kwa karibu wafanyabiashara wenye tabia ya kupandisha bei za bidhaa bila ya sababu za msingi.

Imesema kufanya hivyo kunaathiri na kupingana na hatua yake ya kutoa unafuu wa ushuru wa bidhaa muhimu kwa wafanyabiashara hao hapa nchini.

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo, Ikulu mjini Unguja, katika salamu za kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, alizozitoa kupitia vyombo vya habari.

Dk. Shein alisema inasikitisha kuona licha ya uislamu kuhimiza huruma miongoni mwa binadamu, wapo wafanyabiashara, ambao huutumia mwezi wa Ramadhani kuwa wa kupata faida kubwa kwa kupandisha bei za bidhaa, hasa zile za chakula muhimu, ambazo serikali hupunguza ushuru ili kuwapa nafuu wananchi.

“Nafahamu malalamiko yaliyopo hivi sasa, ambapo wafanyabiashara walipandisha bei za bidhaa kwa kisingizo cha uchaguzi na hadi leo hii bei hizo bado ziko juu,”alisemaDk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema upandishaji bei usio na msingi unakwenda kinyume na malengo ya serikali ya kuanzishwa kwa biashara huru yenye ushindani.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na itahakikisha bidhaa zote muhimu zinazohitajika na kutumika zaidi katika mwezi wa Ramadhani, zinapatikana wakati wote bila ya usumbufu.

Aidha, alisema kwa kuwa Ramadhani ndio mwezi ilipoteremshwa Quraan kupitia Mtume Muhammad (SAW), bidii inahitajika katika kuisoma, kuifahamu na kuhimizana katika kusali swala za fardhi na zile za sunna, hususani nyakati za usiku.

Dk. Shein alisisitiza wajibu wa kuishi kwa kumfanya Mtume Muhammad (S.A.W) kuwa mfano katika kutekeleza ibada mbalimbali ndani ya Ramadhani, ikiwemo kutoa sadaka, kumtaja Mungu, kumuomba msamaha na kufanya ibada ya kukaa msikiti (Itikafu), kuharakisha kufungua wakati unapofika pamoja na kutekeleza sunna ya kula daku.

Mbali na hayo, Dk. Shein alisema ni muhimu ikafahamika kwamba hivi sasa teknolojia imevisogeza vishawishi vingi vinavyoweza kuibatilisha saumu, miongoni mwake vikiwemo mitandao ya simu na intaneti.

Alisema bila ya kujijua, mtu anaweza kujikuta anafanya makosa pale anapoangalia mitandao yenye mambo yasiyopendeza, hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Alisema serikali itaendelea kuchukua tahadhari na hatua mbalimbali kama ilivyotangazwa na Wizara ya Afya, katika kujikinga na maradhi ya milipuko, licha ya kuwa uamuzi huo unaweza kuathiri utamaduni wa kufuturisha, unaoandaliwa na wananchi, taasisi za serikali na binafsi katika kipindi cha Ramadhani.

Katika salamu hizo, Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira na Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA), zifanye kila jitihada ili ziwapatie wananchi maji safi na salama, kwa kutumia magari katika sehemu zote, ambazo zina upungufu  wa maji safi na salama.

No comments:

Post a Comment