Monday 6 June 2016

SAMIA AWATAKA WAJASIRIAMALI KUTUMIA FEDHA KWA NIDHAMU


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka wanawake wajasiriamali nchini kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha ili waweze kujiinua kiuchumi.

Samia alitoa kauli hiyo jana, mjini Dar es Salaam, alipokuwa akizindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Tanzania na Akaunti ya Malaika, inayotolewa na Benki ya Wanawake nchini.

Alisema suala la rasilimali fedha ni mtambuka na linahusisha mambo mbalimbali, hivyo linahitaji nidhamu ya hali ya juu.

“Matumizi mabaya ya rasilimali fedha kwa mambo yasiyokusudiwa huwa ni chanzo kikubwa cha kudorora kiuchumi katika ngazi yoyote ile.
Hata wahenga walisema fedha ni fedheha,” alisema.

Makamu wa Rais alisema mjasiriamali yeyote anahitaji nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya fedha ili kuinua uchumi wa nchi.

“Siku zote mtu mwerevu hawezi kula na mbegu kwa kuwa ukila mbegu utapanda nini? Ni muhimu siku zote ukila, usile na mtaji. Tuwe na tabia ya kuweka akiba, ambayo ikijilimbikiza, inatengeneza mtaji wa biashara nyingine,” alisema na kuongeza:

“Hili ni jambo muhimu sana kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na hata uchumi wa jumuia.”

Aliongeza kuwa wanawake kama wanataka kuinua uchumi wa nchi, wanatakiwa kuheshimu taratibu na mipango wanayopewa na wataalamu.

“Kila mmoja wetu awe na msimamo thabiti wa kupanga matumizi yake ya fedha kulingana na mahitaji yake kwa mpango aliyojiwekea. Fedha ya biashara ibaki kuwa ya biashara na fedha ya matumizi mengineyo itokane na pesa nyingineyo,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu kuteuliwa kwake kuwa mjumbe katika jopo kuu la kumuwezesha mwanamke kiuchumi kwa nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki ya Afrika, alisema nafasi hiyo si yake bali ni ya wanawake wote wa Tanzania.

“Hii si nafasi yangu peke yangu mimi Samia, nafasi hii ni ya wanawake wote wa Tanzania na wa ukanda wa kusini na mashariki mwa Afrika,” alisema.

Samia aliwaomba wanawake hao kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa hatua mbalimbali anazozichukua kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment