Tuesday 22 September 2015

DK. MWAKYEMBE AFYATUKLA TENA KASHFA YA RICHMOND




NA SOLOMON MWANSELE, KYELA

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema kitendo cha CHADEMA kumteua Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, kugombea urais si sahihi na ni kinyume cha demokrasia.
Amesema kimsingi wananchi ambao ni wanachama CHADEMA na UKAWA kwa jumla, hawajatendewa haki kwani walitakiwa kuhusishwa kikamilifu katika mchakato wa kumpata mgombea urais na wabunge.
“Yaani hawa CHADEMA wangefanya kama ambavyo CCM ilimvyompata Dk. John Magufuli, ambaye amepitia huo mchakato kwa kuzunguka nchi nzima, kutafuta wadhamini,” alisema Dk.Mwakyembe.
Dk.Mwakyembe, ambaye ni mgombea wa ubunge jimbo la Kyela aliyasema hayo jana wakati akihutubia wananchi wa Kata ya Lusungo wilayani humo.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, Dk.Magufuli alijieleza kwa wana-CCM, akawekwa kitimoto na kapitia michakato ya kitaifa hatimaye  ndiyo amekuja kupatikana kuwania nafasi hiyo.
“Lakini hawa wa kukaa siku hiyo hiyo, siku hiyo mwanachama wamempa bendera, siku hiyo hiyo …ndo maana imefika mahali unauliza kuna upepo umepita, shetani gani kawapitia, lakini unabaini hakuna cha shetani pale, ni pesa ndiyo pesa imetembea pale,” alisema Dk.Mwakyembe.
Aliongeza kuwa ndio maana sasa hata alama za CHADEMA, zimepotea kwani mwanzoni walikuwa wananyoosha vidole viwili kwa kujiamini, sasa hivi wamebuni alama ya kukoroga na kuwapa tahadhari kuwa wawe makini kwani wanaweza kujikuta wanajipiga ngumi.
Aliwataka CHADEMA na UKAWA kwa jumla, kuiachia CCM kuendelea kutesa mwaka huu na Dk. Magufuli, kwani ndiye chaguo sahihi la Watanzania, hivyo anaomba wampe kura nyingi za ndiyo, ili kuwaadhibu viongozi ambao hawaheshimu demokrasia na wanachama wao.
“Na njia moja tu ya kuwafanya viongozi hawa wa CHADEMA, wasirudie tena kufanya waliyoyafanya safari hii ni kumpa kura zote Dk. Magufuli na kumnyima Lowassa.

ACHENI KUMSHABIKIA HUYU

Dk. Mwakyembe amewataka Watanzania kuacha kushabikia mambo wasiyoyaelewa kuhusu Lowassa.
Alisema Februari 6, mwaka 2008 alisoma taarifa ya uchunguzi bungeni na kuelezea yote, lakini wakaishia kusema vitu viwili moja ikiwa ni kumpa Lowassa uchaguzi.
“Kwanza tulimtaka ajipime mwenyewe, azingatie uchunguzi tuliofanya na matokeo ya uchunguzi wetu, kisha  aangalie iwapo bado ana thamani ya kuendelea kuwa Waziri Mkuu. Kwa maneno mengine tulimtaka ajiuzulu kimya kimya na Bunge litakaa kimya,” alisema Dk.Mwakyembe.
Aliongeza kuwa chaguo lingine alilopewa Lowassa ni kukataa na angefanya hivyo, waliombe Bunge lichukue hatua na likitekeleza hilo Kamati Teule ingemuomba Spika itoe ushahidi kuhusu aliyehusika kuibeba Richmond, kwenye mkataba wa aibu katika historia ya nchi yetu alikuwa ni Lowassa.
Dk. Mwakyembe alisema ushahidi wanao na wangeliomba Bunge ili Lowassa afukuzwe kazi kisha wamfungulie mashtaka ya jinai, lakini cha ajabu alijihami kwa kujiuzulu.
Alisema walikuwa na ushahidi kamili na wangeithibitishia nchi kuwa Lowassa ndiye mhusika, lakini walimshangaa pale aliposimama Bungeni na kumueleza Spika, Samuel Sitta, kuwa ameandika barua kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, kuwa anaachia ngazi.
“Huitaji kuwa profesa wa sheria, huitaji kuwa daktari wa uchumi, ama sayansi ya jamii kuelewa kuwa Lowassa, alikuwa anakiri amehusika, asingeweza kubisha kwani angebisha alijua wazi tutamfikisha kwenye hatima ya kumfukuza na kumfungulia mashtaka,” alisema Dk.Mwakyembe.
Alisema Bunge halijakaa tena na kumsafisha Lowassa, lakini cha ajabu leo watu wanakuja mlango wa nyuma na kusema kina Dk. Mwakyembe walikosea, aliongeza na kuwa watu hao wanaweza wakawa ni watoto wa masikini, hawana mizizi ya utajiri, lakini wamelelewa katika Taifa la Mwalimu Julius Nyerere.
“Tumepata hadhi sawa na matajiri wengine, tuna hadhi, jina langu lina hadhi siwezi kukubali mtu anakuja kuchezea chezea jina langu kwa sababu ana hela. Nitapigana mpaka dakika ya mwisho, kuhakikisha ukweli huu unasikika na kila mtu” alisema.

No comments:

Post a Comment