Tuesday 22 September 2015

CHEYO: LOWASSA HAWEZI KULETA MABADILIKO




Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa chama cha United Democrat Party Taifa (UDP), John Cheyo, amesema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, hana uwezo wa kuleta mabadiliko nchini.
Amesema mwanasiasa huyo ambaye alijiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, alikuwa na wadhifa wa juu nchini,  lakini hakuweza kufanya mabadiliko yoyote hadi alipojiuzulu.
Cheyo, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Itilima mkoani Simiyu, ameonyesha kumuungana mkono mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli.
Akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake zilizofanyika Uwanja wa Mpira wa Kikapu mjini hapa, Cheyo alisema sera yake na chama chake ni kuhakikikisha elimu inatolewa bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne.
Mbali na sera hiyo mbunge huyo alisema kuwa ikiwa wananchi watawapatia ridhaa wagombea ubunge na udiwani wa chama chake, kila kijiji kitapatiwa fedha kwa ajili ya maendeleo ya vijana na kina mama.
Sera hizo zilizotangazwa na Cheyo, zimekuwa zikinadiwa katika maeneo mbalimbali nchini na Dk. Magufuli.
Aidha, Cheyo ameonekana kushangazwa na kauli za Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Lowassa kuwa wataboresha kilimo cha pamba, hali aliyoeleza kuwa ni kudanganya wakulima wa zao hilo.
“Viongozi hawa ni wa ajabu sana…Sumaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 alikuwa wapi kuboresha…mbona alishindwa? Lowassa amekuwa waziri mkuu pia mbona alishindwa?...wakati wakiwa viongozi walisema kuwa hawawezi kuongeza bei ya pamba kutokana na zao hilo kuwa ushirika…sasa leo wataboreshaje?...hao hawastahili  uongozi hao,” alisema.

No comments:

Post a Comment