Mwandishi Wetu, Zanzibar
KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amemtaja ngombea
urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuhusika na vitendo vya
ufisadi na uvufujaji wa fedha za umma wakati akiwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.
Mbali na hilo, amesema Maalim Seif ni kiongozi
atakayesumbua Tanzania na kuiondoa katika amani na utulivu wake kwa kuwa kwa
muda mrefu amejipika na kuwa kupe wa madaraka.
Shaka, alitoa madai hayo juzi katika mkutano wa kampeni wa
kuwanadi wagombea wa CCM, katika jimbo la Mwanakwerekwe mjini Unguja,
zilizofanyika kwenye viwanja vya Ijtmai.
Alisema mgombea huyo urais wa CUF ni kupe na king'ang'anizi
wa madaraka, asiyetosheka kwa nafasi yoyote na kwamba kutamani kwake urais
huenda ana ajenda ya siri dhidi ya
maendeleo ya Zanzibar na mustakabali wake kisiasa , kiuchumi na kiusalama.
"Maalim Seif
ni kupe wa madaraka, hatosheki na hakinai kushika nafasi yoyote hadi awe Rais
wa Zanzibar. Mtazameni kwa makini na mtahadhari naye, hana nia njema, pia ni
hatari kwa mapinduzi yetu, umoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema Shaka.
Alisema mwanasiasa huyo akiwa Waziri Kiongozi katika
miaka ya 1980, alichukua sh. milioni 100 kwa ajili ya kwenda kujitibu
mafindofindo nchini Brunei, lakini hadi sasa hajaonyesha vilelelezo, viambatanisho
au mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo za umma.
“Huyu ni fisadi na mbadhirifu wa mali za serikali,
hastahili kuwa rais,"alisema Shaka,
ambaye Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar.
Alisema uamuzi wa Maalim Seif kwenda kutibiwa nje ya
nchi unatofautiana na ahadi aliyoitoa akiwa serikalini kwamba, angekuwa
akitibiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyoko Unguja.
"Maalim Seif amejisahau na kuamua kutia ulimi wake
puani kwa kukataa kuheshimu ahadi yake ya kutibiwa nchini, sasa anatumia fedha
nyingi za umma nje kila mwaka, ambapo safari yake moja hugharimu mamilioni ya
fedha, ambayo yangeweza kutumika kwa shughuli zingine za maendeleo ya
Wazanzibari na Watanzania kwa jumla,” alieleza Shaka.
Alisema mwanasiasa huyo anaposema ana uwezo wa kuleta
mabadiliko ya kiuchumi na kuleta maisha bora kwa wananchi wote kwa siku mia
moja, anajitafutia umaarufu wa kisiasa na wala hana ubavu wa kutekeleza hayo
kama anavyodai kwenye majukwaa ya kisiasa.
"Awamu ya kwanza chini ya Mzee Abeid Karume iliichukua
Zanzibar miaka minane kuanzia mwaka 1964 hadi 1972, wapinzani walipompiga
risasi, angalau kujenga nyumba za maendeleo, iweje leo Seif anayekwenda kwa
mkongojo alete mabadililo kwa siku mia, vijana wenzangu akili za kuambiwa
changanyeni na zenu," alisema.
Katibu Mkuu huyo alimtupia lawama Maalim Seif na kudai kuwa
mwaka 1995, alitamka kwamba akishinda urais atautambua ufalme uliopinduliwa
Zanzibar mwaka 1964, na kwamba atayazamisha Mapinduzi ya Zanzibar katika mkondo
wa Nungwi.
Shaka alisema kiongozi huyo hana nia njema ya kujenga
umoja na kuleta maelewano, bali anakusudia kushika urais ili kuwagawa wananchi
kwa mapande ya unguja na upemba.
Aliwataka wananchi kuamka, kumtazama na kutompigia kura
za ndiyo mgombea huyo wa CUF na kumhesbu kama ni adui namba moja wa misingi ya
umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, anayepigania kuzorotesha juhudi za
vyama vya ASP na TANU.
"Nchi yetu imepatikana kwa harubu ya Mapinduzi yaliyouangusha usultan uliodumu
miaka zaidi ya 160, tusikubali kupoteza urithi tulioachiwa na bibi, babu,
shangazi na wajomba zetu kwa kukubali ahadi za kusadikika zisizoingia
akilini," aliasa.
Aliwaomba wananchi wa Mwanakwerekwe kuwachagua wagombea
waliosimamishwa na CCM kuwania nafasi mbalimbali zitakazopigiwa kura Oktoba 25,
mwaka huu, wakiongozwa na mgombea urais wa Tanzania Dk. John Magufuli, Dk. Ali
Mohamed Shein kwa urais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.
No comments:
Post a Comment