Wednesday, 1 June 2016

BURIANI SHEIKH MAJID SALEH

MWENYEKITI wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Sheikh Majid Saleh, amefariki dunia.

Sheikh Majid alifariki dunia Jumapili ya Mei 22, mwaka huu na kuzikwa siku hiyo hiyo jioni, katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Mazishi ya Sheikh Majid yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali na wanachama wa CCM wilaya ya Ilala na mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya viongozi wastaafu wa Chama na Serikali.

Miongoni mwa viongozi wastaafu wa serikali waliohudhuria mazishi hayo ni Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilala, Assa Simba, alithibitisha jana kutokea kwa kifo hicho na kuongeza kuwa, walikipokea kwa masikitiko makubwa.

Alisema viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM wilaya ya Ilala, watamkumbuka marehemu Sheikh Majid kutokana na mchango mkubwa aliokuwa akiutoa katika kukiendeleza Chama.

Asaa alisema licha ya kustaafu uongozi wa Chama, Sheikh Majid aliendelea kuwakutanisha wanachama kupitia hafla mbalimbali alizokuwa akiziandaa nyumbani kwake kwa lengo la kubadilishana nao mawazo.

"Sheikh Majid alikuwa mwanachama madhubuti na hodari wa CCM. Licha ya kustaafu uongozi, hakuacha na kusahau kuwakutanisha wanachama katika hafla mbalimbali alizokuwa akiziandaa,"alisema.

Aidha, Asaa alisema marehemu Sheikh Majid alikuwa muumini mkubwa wa dini ya kiislamu na kwamba, alikuwa na utaratibu wa kuandaa hafla mbalimbali za kidini kila mwaka, nyumbani kwake, Kariakoo, Dar es Salaam.

Mbali na kuwa mwanachama mkereketwa wa CCM, Sheikh Majid alikuwa mmoja wa viongozi wa Jumuia ya Kiislamu ya Sunni Jamaat na pia mwanamichezo maarufu.

Enzi za uhai wake, Sheikh Majid alikuwa na utaratibu wa kuzisaidia vifaa vya michezo timu mbalimbali za soka za wilaya hiyo, ikiwemo Manyema, ambayo aliwahi kuifadhili miaka ya 1990.

Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilala mwishoni mwa miaka ya 1990 na kuitumikia nafasi hiyo kwa kipindi kimoja kabla ya kuamua kustaafu.

Baadaye wadhifa huo ulichukuwa na Mikidadi Mahamoud, aliyepokewa kijiti na Karanje Selemani kabla ya nafasi hiyo kuchukuliwa na Asaa Simba.

No comments:

Post a Comment